May 28, 2020 11:43 UTC
  • UN: Kuna uwezekano kumejiri uhalifu wa kivita DRC

Umoja wa Mataifa umetahadahrisha kuwa kuna uwezekano kuwa kumejiri uhalifu wa kivita Kaskazini Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, baada ya watu kadhaa kuuawa na makundi ya watu wenye silaha.

Ofisi ya Pamoja ya Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa (UNJHRO) inmechapisha ripoti inayosema  mauaji, vitendo vya kikatili, ubakaji na vitendo vingine vinavyokiuka sheria za haki za binadamu vimekithiria na vinatekelezwa na wanamgambo wenye silaha Kaskazini Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), hasa kabila la Walendu.

Ripoti hiyo imesema vitendo hivyo vinaweza kuwa uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya binadamu.

Katika ripoti yake, Ofisi ya Pamoja ya Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa (UNJHRO) imesema katika kipindi cha miezi sita iliyopita, watu wasiopungua 296 wameuawa, 151 kueruhiwa na wengine 38 kubakwa, wakiwamo wanawake na watoto.

UNJHRO imesema vitendo hivyo vya kikatili vilitekelezwa na waasi kutoka kabila la Walendu kati ya mwezi Novemba mwaka uliopita na mwezi Aprili mwaka huu.

Baada ya miaka kadhaa ya utulivu, ghasia za kikabila zimeongezeka tangu mwezi Desemba 2017, hasa kutokana na mizozo ya ardhi.

Mkoa wa Ituri Kaskazini Mashariki mwa DRC una utajiri mkubwa wa mali asili kama vile dhahabu, almasi, coltan na mafuta. Mkoa huo umekuwa medani ya mapigano makali baina ya wanamgambo hasa wale wa makabila mawili hasimu ya Hema na Lendu.

Tags

Maoni