May 29, 2020 06:18 UTC
  • Wanamgambo wa Haftar: Uturuki ni hatari kubwa kwa Libya

Msemaji wa wanamgambo wanaojiita "Jeshi la Taifa la Libya" chini ya jenerali muasi Khalifa Haftar amesema kuwa, uingiliaji wa kijeshi wa Uturuki ni hatari sana kwa Libya.

Mtandao wa habari wa al Bawaba News umeripoti habari hiyo ukimnukuu Ahmed al Mismari akisema kuwa, ndege zisizo na rubani za Uturuki zimetumwa katika eneo la Misrata na kwamba wanamgambo wa kundi lake wako tayari kukabiliana na uingiliaji huo wa Uturuki katika masuala ya ndani ya Libya.

Msemaji huyo wa wanamgambo wa Jenerali Khalifa Haftar ameongeza kuwa, jeshi la Uturuki limepata hasara kubwa  na ndio maana vyombo vya habari vya nchi hiyio na waungaji mkono wao vimeamua kueneza uvumi wa uongo kuhusu matukio ya Libya.

Uturuki inashutumiwa kwa kutuma nchini Libya magaidi waliofanya jinai kubwa dhidi ya wananchi na maafisa wa serikali ya Syria.

Jenerali Khalifa Haftar

 

Uturuki inadai kuwa inaisaidia Serikali ya Mwafaka wa Kitaifa iliyoundwa na Umoja wa Mataifa chini ya Waziri Mkuu, Fayes al Sarraj.

Mwaka jana, al Sarraj alikutana na Rais Recep Tayyip Erdogan wa Uturuki mjini Ankara na baada ya hapo Uturuki ilituma wanajeshi wake nchini Libya kuisaidia Serikali ya Mwafaka wa Kitaifa.

Kwa upande wake, wanamgambo wa "Jeshi la Taifa la Libya" wanaungwa mkono na mahasimu wakubwa wa Uturuki yaani Saudi Arabia, Misri, Umoja wa Falme za Kiarabu (Imarati) na baadhi ya nchi za Magharibi.

Waungaji mkono wa wanamgambo hao wametoa tamko la pamoja kuilaani Uturuki kutuma wanajeshi wake huko Libya.

Tags

Maoni