May 29, 2020 06:39 UTC
  • Kansela wa Ujerumani alaumiwa baada ya silaha za nchi hiyo kuonekana zikitumika Libya

Chama cha Kijani ambacho ni moja ya vyama vya upinzani nchini Ujerumani kimemshutumu Kansela wa nchi hiyo Angela Merkel kwa kutoheshimu marufuku ya Umoja wa Mataifa na kumtaka atoe ufafanuzi kuhusu kutumwa silaha za nchi hiyo kwa makundi hasimu nchini Libya.

Kwa mujibu wa televisheni ya al Jazeera ya Qatar, jana Alkhamisi chama cha Kijani cha Ujerumani kilimtaka Merkel atoe maelezo kuhusu ni vipi silaha za Ujerumani zimefika mikononi mwa jenerali muasi, Khalifa Haftar huko Libya ambaye anaongoza kundi linalojiita Jeshi la Taifa la Libya.

Silaha za Wamagharibi ikiwemo Ujerumani zimeangamiza na kufanya uharibifu mkubwa nchini Libya

 

Hivi karibuni vyombo vya habari vya Serikali ya Mwafaka wa Kitaifa ya mjini Tripoli chini ya waziri mkuu Fayez al Sarraj inayotambuliwa kimataifa vilitangaza kuwa, malori kadhaa ya kijeshi yaliyotengenezwa nchini Ujerumani yanawapelekea wanamgambo wa Haftar zana za kijeshi za kukabiiana na mashambulizi ya anga. Hayo yanajiri katika hali ambayo kwa muda mrefu sasa, duru mbalimbali duniani zinailaumu Ujerumani kwa kuchochea mapigano nchini Libya na kutojali vikwazo na marufuku ya kutopeleka silaha katika nchi hiyo iliyoathiriwa vibaya na vita.

Hivi karibuni televisheni ya DW ya Ujerumani iliripoti kwamba, licha ya kuweko madai ya Ujerumaini ya kuheshimu vikwazo na marufuku ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ya kutopelekwa silaha huko Libya, lakini silaha nyingi zinazotumiwa nchini humo zinatokea Ujerumani.

Kwa mujibu wa ripoti ya Wizara ya Uchumi ya Ujerumani, tangu kilipoitishwa kikao cha viongozi wa Libya miezi minne iliyopita, serikali ya Ujerumani imeshapeleka silaha zenye thamani ya dola milioni 331 huko Libya na kuzipa pande hasimu zinazoungwa mkono na nchi zenye uadui mkubwa baina yao za Misri, Uturuki na Umoja wa Falme za Kiarabu (Imarati).

Tags

Maoni