Jun 01, 2020 10:22 UTC
  • Genge la wabeba silaha laua 18 Nigeria, laiba maelfu ya mifugo

Genge la watu waliojizatiti kwa silaha limeshambulia kijiji kimoja huko kaskazini magharibi mwa Nigeria na kuua watu 18 mbali na kuiba maelfu ya mifugo ya wakazi wa kijiji hicho.

Msemaji wa polisi, Gombo Isa amesema watu waliotekeleza shambulizi hilo dhidi eneo la Faskari kaskazini magharibi mwa nchi walikuwa wamebeba silaha nzito huku wengine wakijizatiti kwa mapanga.

Shirika la habari la Reuters limenukuu mashuhuda wa shambulizi hilo wakisema kuwa, wabeba silaha hao wapatao 500 waliwashambulia kiholela wakazi wa kijiji hicho huku wakiwa juu ya pikipiki.

Inasemekana kuwa, baada ya kuvamia eneo la Faskari, watenda jinai hao walielekea katika kijiji cha Sabon Garin katika jimbo la Katsina la kaskazini magharibi mwa nchi na kuua kiongozi wa eneo hilo anayefahamika kaa Abdulhamid Sani aliyekuwa na umari wa miaka 55, baada ya jaribio la kumteka nyara kufeli. 

Wakazi wakitazama maiti za makumi ya watu waliouawa katika jimbo la Sokoto hivi karibuni

Mashuhuda wanasema baada ya kutekeleza ukatili huo, wahalifu hao walikimbilia katika eneo la Batsari. Msemaji wa polisi, Gombo Isa amesema maafisa usalama wameanzisha msako mkali katika msitu mmoja ulioko katika eneo hilo, kwa ajili ya kuwasaka na kuwafikisha mbele ya vyombo vya dola wahalifu hao. 

Haya yanajiri siku chache baada ya watu 60 kuuawa na wengine wengi kujeruhiwa katika shambulizi lililofanywa na kundi jingine la wapanda pikipiki wenye silaha katika vijiji vya Aduwa, Kuzari, Kutama na Masawa katika jimbo la Sokoto, kaskazini magharibi mwa Nigeria. 

Tags

Maoni