Jun 02, 2020 11:34 UTC
  • Duru mpya ya mazungumzo Libya kwa ajili ya kurejesha amani nchini humo

Vita vya ndani vingali vinaendelea nchini Libya na makundi mawili makuu hasimu yamekuwa yakitwaa na kufukuzwa katika maeneo ya kistratijia kwa zamu. Hali hiyo pia imezidisha uingiliaji kati ya nchi za kigeni katika masuala ya ndani ya Libya.

Sambamba na mapigano hayo, kunafanyika jitihada za kimataifa za kurejesha amani na utuulivu katika nchi hiyo iliyoraruriwa na vita vya wenyewe kwa wenyewe. Katika mkondo huu ofisi ya mwakilishi wa Umoja wa Mataifa nchini Libya UNSMIL imetangaza kuwa pande mbili hasimu yaani Serikali ya Mwafaka wa Kitaifa na kundi la jenerali muasi, Khalifa Haftar zimekubaliana kuanza duru ya tatu ya mazungumzo ya kamati ya pamoja ya masuala ya kijeshi inayojulikana kwa jina la 5+5. Lengo la mazungumzo hayo ni kusimisha vita na mapigano. Duru ya kwanza na ya pili ya mazungumzo ya kamati ya 5+5 ilifanyika mwezi Februari katika mji wa Geneva chini ya usimamizi wa mjumbe wa zamani wa UN katika masuala ya Libya, Ghassan Salamé. Mazungumzo hayo yaliwakutanisha meza moja maafisa watano wa Serikali ya Mwafaka wa Kitaifa na wengine tano wa kundi linalojiita Jeshi la Taifa la Libya chini ya uongozi wa jenerali muasi, Khalifa Haftar. Hata hivyo mazungumzo hayo yalisimamishwa baada ya kundi la Haftar kukiuka makubaliano ya usitisha vita na kuendeleza hujuma na mashambulizi. 

Mwenyekiti wa sasa wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, Sven Jürgenson anasema: Yanayojiri Libya yanatia wasiwasi kwa sababu makubaliano ya usitisha vita yamekuwa yakikiukwa haraka na wapiganaji wa Khalifa Haftar. 

Sven Jürgenson

Vita vya Libya vimeshadidi zaidi katika miezi ya hivi karibuni. Jeshi la Serikali ya Mwafaka wa Kitaifa inayotambuliwa rasmi na jamii ya kimataifa limeanzisha mashambukizi na hujuma kali katika maeneo mbalimbali ya Libya kwa shabaha ya kuwashinda wapiganaji wa Haftar na limefanikiwa kupata ushindi katika baadhi ya maeneo ya Libya. Wakati huo huo jeshi la Haftar linalosaidiwa na nchi kama Saudi Arabia, Imarati na Misri limezisha hujuma dhidi ya ngome za Serikali ya Mwafaka wa Kitaifa, suala linaloifanya Libya kuwa medani ya vita vya niaba. Hii ni licha ya kwamba, wataalamu wa masuala ya kijeshi na kisiasa wanaamini kuwa, mgogoro wa Libya hauwezi kutatuliwa kwa mtutu wa bunduki.   

 Taarifa iliyotolewa na mwakilishi wa Umoja wa Mataifa nchini Libya inasema kuwa: Kurejea pande mbili hasimu katika meza ya mazungumzo ni jibu mwafaka kwa matakwa ya Walibya waliowengi ambao wanatarajia kuishi kwa amani haraka iwezekanavyo.

Vita vya ndni Libya

Vita vya kuwania madaraka nchini Libya vinaendelea huku Serikali ya Mwafaka wa Kitaifa ikitangaza kuwa, inakaribia kupata ushindi mkubwa. Jeshi la Haftar pia linaendeleza mashambulizi kwa shabaha ya kuuteka mji wa Tripoli. Sambamba na hayo Libya na Walibya wanaendelea kuhangaika kutokana na kuharibiwa taasisi za mafuta ya petroli, kupungua uuzaji nje wa bidhaa hiyo, wimbi la maambukizi ya corona na uingiliaji kati wa nchi za kigeni katika masuala ya nadni ya nchi yao. Mikono na nyayo za miguu ya nchi mbalimbali kama Saudi Arabia, Imarati, Misri, Marekani, Uturuki na hata Russia inaonekana waziwazi katika vita na machafuko ya sasa ya Libya. Nchi hizo zinawania kumega keki ya Libya yenye utajiri kubwa wa mafuta na zinaoina hali ya sasa nchini humo kuwa inafaa kwa ajili ya kuimarisha satua na ushawishi wao wa kisiasa katika nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika. Kwa msingi huo zinakiuka na kukanyaga marufuku ya silaha ya Umoja wa Mataifa dhidi ya Libya.

Sasa kumeripotiwa kuanza duru ya tatu ya mazungumzo ya amani kuhusiana na Libya. Japokuwa tajiriba na uzoefu wa huko nyuma vimeonyesha kuwa, mazungumzo kama haya ambayo pande zake mbili hazina azma ya kweli ya kutekeleza maamuzi yake, hayawezi kufua dafu. Hata hivyo kuna matumaini japo kidogo kwamba mara hii pande hasimu zitatilia maanani ukweli wa mambo na kutayarisha amzingira ya kupatikana makubaliano ya amani ya kudumu katika nchi hiyo ya Kiafrika.   

Tags

Maoni