Jun 03, 2020 03:55 UTC
  • Rais wa Ghana: Natumai mauaji ya Floyd yatachochea mabadiliko Marekani

Rais wa Ghana ameashiria kuhusu mauaji ya kutisha ya Mmarekani mmoja mwenye asili ya Afrika katika mji wa Minneapolis nchini Marekani na kusema kuwa, "natumai kifo cha George Floyd kitakuwa chachu ya madiliko ya kudumu ya matatizo ya chuki na ubaguzi."

Nana Addo Dankwa Akufo-Addo ameeleza juu ya kushtushwa na kusikitishwa kwake na mauaji ya Floyd na kueleza bayana kuwa, watu weusi kote duniani wameghadhabishwa na kusikitishwa na mauaji hayo ya kikatili dhidi ya mtu mweusi ambaye hakuwa na silaha yoyote.

Amesema taifa la Ghana limesimama na Wamarekani wenye asili ya Afrika katika kipindi hiki kigumu cha simanzi. Rais wa Ghana amebainisha kuwa: Si sawa katika karne hii ya 21, Marekani, kitovu cha demokrasia, inaendelea kukabiliana na tatizo la ubaguzi wa rangi unaofanyika kwa mpangilio maalumu.

Maandamano ya kulaani ubaguzi na ukatili wa polisi ya Marekani dhidi ya raia weusi

Rais Nana Akufo-Addo  wa Ghana ameongeza kuwa, mauaji hayo ya kutisha ya Mmarekani mweusi yanabeba taswira ya hali halisi ya kila siku inayoumiza, na kumbukumbu yenye sura ya kutisha.

Mei 25, afisa mmoja mzungu wa jeshi la polisi la Marekani alimuua kikatili George Floyd, Mmarekani mmoja mwenye asili ya Afrika katika mji wa Minneapolis, ukatili ambao umezusha wimbi kubwa la maandamano na machafuko katika kona zote za Marekani, na hivi sasa maandamano hayo yameenea katika nchi mbalimbali duniani.

Tags

Maoni