Jun 06, 2020 07:53 UTC
  • Kiongozi wa kundi la al-Qaeda kaskazini mwa Afrika auawa nchini Mali

Waziri wa Ulinzi wa Ufaransa ametangaza kuwa jeshi la nchi hiyo ya Ulaya limefanikiwa kumuua kiongozi wa mtandao wa kigaidi wa al-Qaeda katika eneo la Maghreb kaskazini mwa Afrika (Aqim) huko nchini Mali.

Florence Parly amesema Abdelmalek Droukdel na wasaidizi wake kadhaa waliuawa wakati wa operesheni ya kijeshi iliyofanyika mnamo Juni 3 huko kaskazini mwa Mali.

Amebainisha kuwa, operesheni hiyo ilitekelezwa kaskazini mwa eneo la Adrar des Ifoghas, umbali wa kilomita 80 mashariki mwa Tessalit, karibu na mpaka na Algeria.

Ufaransa ina wanajeshi zaidi ya 5,000 katika eneo la Sahel la Afrika linalozijumuisha nci za Mauritania, Mali, Burkina Faso, Niger na Chad.

Hii ni katika hali ambayo, mwezi uliopita, makumi ya wanajeshi wa Mali waliuawa katika shambulio la magaidi dhidi ya kambi moja ya jeshi katika eneo la Bamba jimboni Gao, kaskazini mwa nchi.

Baadhi ya wanachama wa mtandao wa kigaidi wa al-Qaeda

Katika miaka ya hivi karibuni nchi ya Mali imekuwa ikikabiliwa na mashambulizi ya mara kwa mara ya makundi ya waasi na magaidi wa makundi ya al-Qaeda na Daesh (ISIS). 

Mwaka 2013 Umoja wa Mataifa ulituma kikosi cha askari wa kimataifa cha MINUSMA  nchini Mali kwa ajili ya kukabiliana na waasi na wanamgambo hao kikishirikiana na wanajeshi wa Ufaransa. Hata hivyo askari hao wa UN na wa Ufaransa hawajafanikiwa kurejesha amani na utulivu  nchini Mali na nchi hiyo bado inakabiliwa na tishio kubwa la makundi ya kigaidi yanayofanya mauaji ya mara kwa mara.  

Tags