Jun 11, 2020 08:04 UTC
  • Wananchi wa Senegal waandamana kulaani ubaguzi wa rangi Marekani

Wananchi wa Senegal wamefanya maandamano kulaani ubaguzi wa rangi na ukatili wa polisi ya Marekani dhidi ya raia weusi wa nchi hiyo.

Kwa mujibu wa shirika la habari la IRIB, maandamano hayo yamefanyika katika mji mkuu wa Senegal, Dakar.

Baadhi ya waandamanaji hao walikuwa wambeba mabango yenye jumbe mbalimbali za kulaani jinai hiyo. Baadhi ya mabango hayo yalikuwa yameandikwa: Maisha ya weusi ni muhimu na komesha ubaguzi.

Kadhalika waandamanaji hao walipiga goti, kuashiria mbinu ya kikatili iliyotumiwa na polisi mmoja mzungu wa Marekani kumuua Mmarekani mweusi mwishoni mwa mwezi uliopita.

Mapema mwezi huu, miji mikuu ya Kenya na Nigeria ilishuhudia pia maandamano ya kulaani ubaguzi huo wa rangi na mauaji ya George Floyd, raia wa Marekani mwenye asili ya Afrika aliyeuliwa kikatili na polisi mmoja mzungu katika mji wa Minneapolis, katika jimbo la Minnesota nchini Marekani mwishoni mwa mwezi uliopita.

Maandamano ya kulaani ubaguzi wa rangi yamashuhudiwa katika nchi mbalimbali duniani

Baada ya polisi mzungu kumuua kinyama George Floyd, Mmarekani mweusi mnamo Mei 25, raia wa nchi hiyo wamekuwa wakimiminika mabarabarani kulaani jinai hiyo kwa karibu wiki mbili sasa.

Maandamano hayo ya kulaani ubaguzi wa rangi na ukatili wa polisi ya Marekani hivi sasa yameenea na kusambaa katika nchi mbalimbali duniani zikiwemo za Ulaya na Afrika.

 

Tags