Jun 17, 2020 13:55 UTC
  • Magufuli akipokea fomu za kuwania urais 2020
    Magufuli akipokea fomu za kuwania urais 2020

Rais John Magufuli wa Tanzania ambaye ni Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) asubuhi leo Jumatano amechukua fomu ya kuwania kinyang’anyiro cha urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika uchaguzi mkuu utakaofanyika mwaka huu.

Magufuli amekabidhiwa fomu hiyo na Kuu Mkuu wa CCM Taifa, Dkt. Bashiru Ally, kwenye makao makuu ya chama hicho mkoani Dodoma.

Akizungumza baada ya kukabidhiwa fomu, Magufuli amesema anaanza mapema mchakato wa kutafuta wadhamini ili awahi kurejesha fomu hiyo mapema.

Mwenyekiti huyo wa CCM amesema amekuwa akipigiwa simu na makada wa chama hicho, ambao wamemwahidi kumdhamini.

“Naomba nianze zoezi hili la kutafuta wadhamini, nitaenda mikoa yote kwa sababu nimekuwa nikipigiwa simu wakisema wanataka kunidhamini hivyo nitarejesha fomu yangu kwa wakati,” amesema John Pombe Magufuli.

Kwa upande wa Zanzibar joto la uchaguzi wa rais wa Serikali ya Mapinduzi limezidi kupamba moto baada ya Waziri wa Ulinzi wa Tanzania, Hussein Mwinyi kujitosa uwanjani na kuchukua fomu kwa ajili ya kugombea nafasi hiyo.

Hussein Mwinyi akichukua fomu za kugombea urais Zanzibar.

Dkt. Hussein Mwinyi amechukua fomu kwa lengo la kuwania nafasi ya Urais wa Zanzibar katika ofisi za chama cha Mapinduzi (CCM) Kisiwandui mjini Unguja mapema Leo.

Hussein Mwingi mbaye ni mtoto wa rais mstaafu wa Tanzania, Ali Hassan Mwinyi amekuwa mgombea wa tano kuchukua fomu akitanguliwa na Mbwana Bakari Juma, Mbwana Yahya Mwinyi, Omar Sheha Mussa na Balozi Ali Karume ambaye ni mtoto wa rais wa kwanza wa Zanzibar, Amani Abeid karume.

Balozi Ali Karume

Zoezi la kuchukua fomu kwa wagombea wa Urais kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi upande wa Tanzania Bara na Zanzibar lilianza tarehe 15 mwezi huu na litakamilika tarehe 30.

Tags

Maoni