Jun 25, 2020 07:56 UTC
  • Rais wa Senegal yuko karantini baada ya kutangamana na mwenye corona

Rais Macky Sall wa Senegal amejiweka katika karantini baada ya kutagusana na mtu mwenye maradhi ya COVID-19.

Kanali ya televisheni ya taifa ya RTS1 imeripoti kuwa, Sall ameanza karantini hiyo ya siku 15 kuanzia jana Jumatano.

Taarifa ya Ofisi ya Rais wa Senegal hata hivyo imesisitiza kuwa, tayari Sall amefanyiwa vipimo na kupatikana kuwa hajaambukizwa virusi vya corona, lakini binafsi ameamua kujiweka karantini baada ya kukutangamana na mgonjwa wa corona.

Hali ya maambukizi ya virusi vya corona nchini Senegal hususan katika mji mkuu wa nchi hiyo imewapelekea maafisa wa afya na tiba wa nchi hiyo kubainisha wasiwasi wao.

Mapema mwezi huu, Abdoulaye Diouf Sarr, Waziri wa Afya wa Senegal alieleza wasiwasi wake mkubwa kuhusu hali ya maambukizi ya corona nchini humo hususan katika mji mkuu Dakar.

Hali ya corona nchini Senegal inatisha

Takwimu za Wizara ya Afya ya Senegal zinaonyesha kuwa, tokea Machi 2 hadi sasa watu 6,129 wameambukizwa corona nchini humo na wengine 93 wameaga dunia. Zaidi ya nusu ya watu walioambukizwa virusi vya corona wameripotiwa katika mji mkuu Dakar.

Habari njema ni kuwa, watu 4,072 waliokuwa wamembukizwa virusi vya corona nchini humo wamepata afueni na kuruhusiwa kuondoka hospitalini.

 

Tags