Jul 02, 2020 04:35 UTC
  • Benki ya Dunia: Tanzania ni taifa lenye uchumi wa kipato cha kati

Benki ya Dunia imeiorodhesha Tanzania katika orodha ya nchi za uchumi wa kipato cha kati.

Hatua hii inajiri miaka mitano kabla ya malengo ya maendeleo ya taifa hilo ambapo ilikuwa imelenga kuafikia kiwango hicho kufikia 2025.

Na kufuatia hatua hiyo Rais wa Tanzania John Pombe Magufuli amewapongeza wananchi wa taifa hillo kwa mafanikio hayo.

Katika chapisho aliloliweka katika mtandao wake wa twitter rais Magufuli amesema kwamba : ''Huu ni ushindi mkubwa na kazi kubwa tumeifanya, tulipanga kuingia katika uchumi wa kati ifikiapo mwaka 2025 lakini tumefanikiwa.''

Rais John Pombe Magufuli wa Tanzania anasifiwa kimataifa kutokana na kupambana na ufisadi na kuimarisha uchumi wa nchi yake

Kulingana na mtaalamu wa masuala ya kiuchumi kutoka Tanzania Deus Kibamba benki hiyo hutazama pato la taifa kwa mfano kupitia jumla ya utajiri wa raslimali na ule wa kifedha na kugawanya na idadi ya watu wa Tanzania.

Licha ya kupongezwa kwa hatua mbalimbali za maendeleo zilizochukuliwa na serikali yake, zikiwemo za kustawisha miundomsingi ya kiuchumi na kupambana na ufisadi, Rais John Pombe Magufuli wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania anakosolewa kuwa anaminya na kukandamiza demokrasia sambamba na kuendesha kampeni ya kuua vyama vya upinzani katika nchi hiyo ya Afrika Mashariki.

Wanasiasa wa upinzani wanadai kuwa serikali ya sasa ya Rais Magufuli imeweka mazingira magumu ya kufanya mikutano ya kisiasa na kukandamiza demokrasia.

Maoni