Jul 02, 2020 07:39 UTC
  • Jeshi lasambazwa Addis Ababa baada ya mauaji ya watu 80

Jeshi la Ethiopia limesambazwa katika mji mkuu wa nchi hiyo, Addis Ababa kwa shabaha ya kudhibiti machafuko yaliyosababisha vifo vya watu wasiopingua 80.

Watu walioshuhudia wanasema vikosi vya jeshi la Ethiopia vimesambazwa katika maeneo mbalimbali ya mji mkuu, Addis Ababa baada ya magenge yanayobeba silaha baridi kuvamia makazi ya raia  na kwamba milio ya risasi ilikuwa ikisika hapa na pale.

Vilevile kumeripotiwa mapigano baina ya vijana wa kabila la Oromo na vijana kutoka makabila mengine mjini humo.

Machafuko ya sasa nchini Ethiopia yaliibuka Jumanne iliyopita baada ya mwanamuziki na mwanaharakati mashuhuri nchini humo, Haacaaluu Hundeessaa kuuawa kwa kupigwa risasi na watu wasiojulikana mjini Addis Ababa Jumatatu usiku.

Haacaaluu Hundeessaa

Machafuko hayo sasa yamepanuka zaidi hadi katika maeneo mengine ya Ethiopia hususan katika mkoa wa Oromiya ambako polisi inasema watu wasiopinga 50 wameuawa.

Polisi katika mkoa huo pia imemtia nguvuni kiongozi wa chama cha upinzani, Bekele Gerba na vilevile mwanaharakati wa kisiasa na mmiliki wa vyombo vya habari, Jawar Mohammed, suala ambalo wachambuzi wa mambo wanasema yumkini likazidisha ghasia na machafuko.

Wakari huo huo Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed amezituhumu baadhi ya nchi za kigeni kwamba zinachochea machafiko nchini kwake kwa shabaha ya kuzuia ukamilishaji wa ujenzi wa Bwawa la Renaissance.  

Ujenzi wa Bwawa la Renaissance unaofanyika nchini Ethiopia juu ya maji ya Mto Nile umezusha mgogoro mkubwa baina ya nchi hiyo na nchi za Misri na Sudan.

Misri inatambua ujenzi wa bwawa hilo kuwa ni tishio kwa usalama wake wa kitaifa kwa sababu karibu asilimia 90 ya mahitaji yake ya maji yanadhaminiwa kutokana na Mto Nile.

Ethiopia inakanusha madai hayo ikisema Bwawa la Renaissance ni muhimu sana kwa ajili ya ustawi wa maendeleo ya taifa hilo.

Tags

Maoni