Jul 03, 2020 12:46 UTC
  • Sababu zilizoifanya Tanzania kufikia uchumi wa kipato cha kati

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imesema kuwa, utekelezaji wa miradi mikubwa ya kimkakati iliyobuni ajira kwa Watanzania wengi ni kati ya vitu ambavyo viliivutia Benki ya Dunia na kuifanya kuitangaza nchi hiyo kama taifa lenye kipato cha kati.

Hayo yameelezwa na Dakta Hassan Abbasi, msemaji wa serikali ya Tanzania ambye amebainisha kuwa, takwimu za kipato cha waliopata ajira ndio sehemu kubwa iliyochukuliwa na Benki ya Dunia kuthibitisha kwamba pato la Watanzania limeongezeka.

Afisa huyo wa serikali alitaja ujenzi wa mradi wa umeme wa Rufiji wa megawati 2500 kama mojawapo ya mambo yaliyosababisha kuimarika kwa uchumi wa taifa hilo, mradi ambao umebuni zaidi ya ajira 3500.

''Katika miaka 59 tunayoelekea ya Uhuru na katika miaka mitano ya uongozi wa Rais Magufuli kama kuna eneo tumewekeza kwa kiasi kikubwa na limesaidia sana kuchemsha uchumi ni katika ujenzi ambao wengine wanaita maendeleo ya vitu, amesema afisa huyo wa serikali.

Rais John Pombe Magufuli wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Mbali na uongozi thabiti wa Rais Magufuli katika kudhibiti matumizi ya fedha na kukabiliana na ufujaji wake, Bwana Abbas amesema kwamba, taifa la Tanzania limeimarika kiviwanda hali ya kwamba lina karibia viwanda 60 tangu lilipojipatia Uhuru, huku uongozi wa rais Magufuli ukifanikiwa kuanzisha zaidi ya viwanda elfu nane katika kipindi cha miaka mitano ya uongozi wake.

Benki ya dunia siku ya Jumatano iliiorodhesha Tanzania katika orodha ya nchi za uchumi wa kipato cha kati. Hatua hiyo inajiri miaka mitano kabla ya malengo ya maendeleo ya taifa hilo ambapo ilikuwa imelenga kufikia kiwango hicho kufikia 2025.

Maoni