Jul 04, 2020 07:51 UTC
  • Tanzania yafunga vituo vya COVID-19 kwa kukosa wagonjwa wapya

Wizara ya Afya ya Tanzania imetangaza habari ya kufunga vituo 74 kati ya 85 vilivyokuwa vimetengwa makhsusi kwa ajili ya wagonjwa wa COVID-19 baada ya kukosa kupokea wagonjwa wapya, huku ikisisitiza kuwa janga la corona limepungua kwa kiasi kikubwa nchini humo.

Waziri wa Afya wa Tanzania, Ummy Mwalimu amesema hayo katika taarifa ya jana Ijumaa, baada ya kufunga kambi ya wagonjwa wa COVID-19 ya Lulanzi katika wilaya ya Kibaha mkoa wa Pwani. Amesema, "mgonjwa wa mwisho wa corona katika kituo hiki cha Lulanzi aliruhusiwa kwenda nyumbani mnamo Mei 26 na tokeo wakati huo, kambi hii haijapokea mgonjwa mwingine."

Amesema nchi hiyo ya Afrika Mashariki imebaki na kambi 11 za wagonjwa wa COVID-19 ambazo pia zipo katika mchakato wa kufungwa kutokana na kupungua kwa kiasi kikubwa kesi za maambukizi ya ugonjwa huo hatari nchini humo. Amesema vituo hivyo kwa sasa vinatoa huduma nyinginezo za afya.

Hata hivyo Waziri wa Afya wa Tanzania amewaonya wananchi dhidi ya kupuuza kanuni na protokali za afya ili kuzuia kutokea wimbi jipya la maambukizi kama inavyoshuhudiwa katika nchi nyingine duniani.

Waziri wa Afya wa Tanzania, Ummy Mwalimu

Wizara ya Afya ya Tanzania ilitoa takwimu za corona mara ya mwisho mnamo Aprili 29 ambapo ilitangaza kuwa imethibitisha kesi 509 na vifo 21 vya corona.

Serikali ya Dar es Salaam ilitangaza kufunguliwa shule zote nchini humo mwishoni mwa mwezi uliopita wa Juni, mbali na kuruhusu nchini humo ndege za kimataifa na kufungua shughuli za kiuchumi na kijamii.  

Tags

Maoni