Jul 04, 2020 11:39 UTC
  • Magaidi kadhaa wa Boko Haram wauawa kaskazini mashariki mwa Nigeria

Jeshi la Nigeria limetangaza habari ya kuuawa magaidi kadhaa wa Boko Haram katika msitu wa Sambisa wa kaskazini mashariki mwa nchi hiyo.

Taarifa rasmi ya jeshi la Nigeria imesema kuwa, magaidi wengi wa Boko Haram wameuawa katika shambulio la anga lililofanywa na jeshi hilo katika msitu wa Sambisa, wa jimbo la Borno la kaskazini mashariki mwa nchi hiyo.

Msemaji wa jeshi la Nigeria, John Enenche amethibitisha habari hiyo na kusema katika taarifa hiyo kuwa, wanajeshi wa serikali wamefanikiwa pia kuteketeza sehemu ya mikutano ya magaidi hao katika eneo la Mainyakare kwenye msitu huo.

Msitu wa Sambisa ndiyo maficho makuu ya magaidi wa Boko Haram na ndiko wanakofanyia mazoezi yao kabla ya kuvamia vijiji na maeneo mengine ya Nigeria na kushambulia kigaidi raia wa kawaida.

Msitu wa Sambisa huko Borno, kaskazini mashariki mwa Nigeria

 

Enenche amesema, operesheni hiyo imefanyika baada ya kukusanywa taarifa za kiintelijensia  na ni muendelezo wa mashambulizi ya anga yanayolenga kusambaratisha maficho na vituo vikuu vya genge hilo la ukurufishaji.

Kwa muongo mzima sasa eneo la kaskazini mashariki mwa Nigeria limekuwa uwanja wa mashambulizi ya magaidi wa Boko Haram ambao mwaka 2014 waliteka nyara mamia ya wasichana katika shule moja ya sekondari mjini Chibok.

Kundi la Boko Haram ambalo maana yake ni "Elimu za Magharibi ni Haramu" ni genge la kigaidi na ukufurishaji lenye mitazamo potofu kuhusu mafundisho matukufu ya Uislamu na limekuwa likifanya jinai na ukatili mkubwa kwa watu wa kawaida hata Waislamu.

Maoni