Jul 05, 2020 09:19 UTC
  • Abdelmadjid Tebboune
    Abdelmadjid Tebboune

Rais Abdelmadjid Tebboune wa Algeria amesema kuwa, hali inayoshuhudiwa sasa nchini Libya inafanana na ile ya Syria kutokana na nchi kadhaa kuingilia masuala ya ndani ya nchi hiyo.

Abdelmadjid Tebboune amesema, kuna uwezekano Libya ikatumbukia katika hali mbaya zaidi ya ile ya Syria iwapo hakutapatikana makubaliano ya kusitisha vita kwa shabaha ya kuanzisha serikali mpya itakayotokana na maamuzi ya wananchi.

Rais wa Algeria ametahadharisha kwamba, Libya inaweza kutumbukia katika hali mbaya zaidi ya ile ya Syria na kuwa Somalia mpya barani Afrika.

Amesema anachelea kwamba makabila ya Libya yataanza kujizatiti kwa silaha na wakati huo Libya itakuwa na hali inayoshabihiana na ile ya Somalia.

Machafuko ya ndani Libya

Siku mbili zilizopita mjumbe maalumu wa zamani wa Umoja wa Mataifa nchini Libya alizilaumu nchi zinazotekeleza siasa za nyuso mbili katika kadhia ya Libya na kusisitiza kuwa, baadhi ya wanachama wa Baraza la Usalama wanamuunga mkono jenerali muasi Khalifa Haftar na kuvunja nguvu juhudi za Umoja wa Mataifa za kuutatua mgogoro wa Libya.

Ghassan Salamé ameongeza kuwa, Khalifa Haftar ambaye anaongoza wanamgambo wanaojiita Jeshi la Taifa Libya, aliivamia na kuishambulia Tripoli akiungwa mkono na sehemu kubwa ya nchi wanachama wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.

Tags

Maoni