Jul 06, 2020 11:19 UTC
  • GNA Libya yaapa kujibu mapigo kwa waliokishambulia kituo cha anga cha al-Watiya

Naibu Waziri wa Ulinzi wa Serikali ya Muafaka wa Kitaifa ya Libya (GNA) amesema, vikosi hivyo vitajibu mapigo katika wakati na mahali mwafaka kwa waliohusika na shambulio dhidi ya kituo cha anga cha al-Watiya.

Akithibitisha kushambuliwa kituo hicho kilichokombolewa hivi karibuni na vikosi vya ulinzi vya GNA kutoka mikononi mwa kundi linalojiita Jeshi la Taifa la Libya LNA linaloongozwa na Khalifa Haftar, Naibu Waziri wa Ulinzi wa GNA Salah al-Namrush amesema katika taarifa na pasi na kutaja nchi maalumu, kwamba kituo hicho kilishambuliwa katika hujuma iliyofanywa usiku wa kuamkia jana Jumapili na ndege za kile alichokitaja "kikosi cha anga cha kigeni" kinachounga mkono jinai za kivita zinazofanywa na Haftar.

Khalifa Haftar

Katika taarifa yake hiyo, al-Namrush, mbali na kutishia kwamba vikosi vya GNA vitachukua hatua dhidi ya kundi la Khalifa Haftar na waitifaki wake wa kikanda na kimataifa, amesema: Hujuma hiyo dhidi ya kituo cha anga cha al-Watiya haitaathiri mwenendo wa matukio na mapigano yanayoendelea au kubadilisha stratejia ya serikali ya Muafaka wa Kitaifa, inayotilia mkazo udharura wa kukombolewa na kudhibitiwa maeneo yote ya nchi hiyo.

Kituo cha anga cha al-Watiya, kilichoko umbali wa kilomita 140 kutoka mji mkuu wa Libya, Tripoli,  kilikombolewa na vikosi vya GNA kutoka mikononi mwa wapiganaji wa kundi la LNA tarehe 18 Mei mwaka huu.../

Tags

Maoni