Jul 06, 2020 11:25 UTC
  • Rais Kenyatta alegeza hatua kwa hatua sheria za kukabiliana na corona Kenya

Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta amelegeza kwa kiasi fulani sheria kali zilizokuwa zimewekwa kwa ajili ya kukabiliana na maambukizi ya ugonjwa wa COVID-19 ambapo umeua watu 150 kufikia sasa nchini humo.

Akilihutubia taifa leo Jumatatu katika Jumba la Harambee jijini Nairobi, Rais Kenyatta ametangaza kuondoa marufuku ya safari ya watu kuingia au kutoka katika kaunti za Nairobi, Mombasa na Mandera kuanzia kesho Jumanne.

Hata hivyo amesema kuwa agizo la kutotoka nje kuanzia saa tatu usiku hadi saa kumi alfajiri litaendelea kuwepo kwa kipindi cha siku 30 zijazo.

Vile vile, Rais Uhuru Kenyatta amesema makanisa na misikiti itafunguliwa lakini waumini wasiozidi 100 ndio watakaoruhusiwa kuhudhuria ibada na kwa muda usiozidi saa moja. Shule za Jumapili na madrasa zitasalia kufungwa kwa muda wa siku 30. 

Hali kadhalika Rais wa Kenya amesema safari za ndege za ndani ya nchini zitaanza Julai 15, huku zile za kimataifa zikitazamiwa kuanza Agosti Mosi, lakini kwa kufuata protokali za kiafya.

Safari za ndege za kimataifa kurejea Kenya kuanzia Agosti Mosi, lakini kwa kufuata protokali za kiafya

Rais Kenyatta amelegeza sheria hizo za kudhibiti maambukizi ya virusi vya corona katika hali ambayo, jana Jumapili, Wizara ya Afya ya nchi hiyo ilisema watu karibu elfu nane wameambukizwa virusi hivyo tangu mwezi Machi mwaka huu hadi sasa, mbali ya maradhi hayo hatarishi ya kuambukiza kuua Wakenya 150 kufikia jana.

Aidha Rais wa Kenya amechukua uamuzi huo siku chache baada ya wanasayansi nchini humo kueleza baada ya kupima damu iliyotolewa kwa ajili ya protini inayotumika kwenye mfumo kinga kwamba, karibu Wakenya milioni 2.6 tayari wamekumbwa na virusi vya corona.../

 

Tags

Maoni