Jul 07, 2020 11:06 UTC
  • Nchi za Afrika zaamua kufungua safari za ndege licha ya ongezeko la kesi za COVID-19

Kesi za ugonjwa wa corona zinaendelea kuongezeka barani Afrika, hata hivyo nchi mbalimbali za bara hilo zimetangaza kufungua tena viwanja vyao vya ndege kwa ajili ya safari za kimataifa. Hiyo ni katika hali ambayo hadi hivi sasa bara la Afrika limesharekodi kesi laki nne na 63 elfu za COVID-19.

Nchi za Afrika zina chaguo gumu sasa hivi kutokana na kasi ya maambukizi ya corona, lakini pia zinahitajia safari za ndege, watalii na biashara na madola ya kigeni. Tatizo linakuja pale tunapozingatia kuwa, safari hizo za kimataifa ndizo waenezaji wakuu wa ugonjwa COVID-19  barani humo. Iwapo nchi za Afrika zitaendelea kufunga anga zao, itabidi zikubali kupata hasara kubwa za kiuchumi huku baadhi ya nchi hizo zikiwa na haja kubwa pia ya misaada ya kibinadamu.

Televisheni ya CGTN ya nchini China imetangaza kuwa, sehemu kubwa ya nchi 54 za Afrika zilitangaza kufunga anga zao kama njia ya kukabiliana na janga la corona. Hatua hiyo ilikuwa ni sawa na kutafuta muda wa kujiandaa kukabiliana vizuri na janga hilo lililoiathiri dunia nzima. Hata hivyo jambo hilo lilikwamisha juhudi za kuwafikishia matibabu na chanjo watu wa maeneo mbalimbali ya Afrika za magonjwa mbalimbali. 

Maambukizi ya corona barani Afrika

 

Kwa mujibu wa televisheni hiyo, nchi za Afrika zimekuwa na idadi ndogo sana ya safari za ndege tangu kuanza janga la corona. Kuna wakati maeneo ya magharibi na katikati mwa Afrika yalikuwa na safari moja tu ya ndege kwa siku. 

Sasa hivi Rais wa Senegal ametangaza kuwa safari za ndege zitaanza nchini humo tarehe 15 mwezi huu wa Julai. Nchi 15 waanachama wa Jumuiya ya Kiuchumi ya Magharibi mwa Afrika zinatarajiwa kuanzisha safari za kimataifa za ndege tarehe 21 mwezi huu wa Julai. Nigeria kwa upande wake ilianzisha safari za ndani za ndege tarehe 8 Julai huku Kenya na Rwanda zikipanga kuanzisha safari hizo tarehe Mosi mwezi ujao wa Agosti.  

Maoni