Jul 13, 2020 10:40 UTC
  • Watu 11 wauawa katika maandamano nchini Mali; Rais ashinikizwa kujiuzulu

Watu wasiopungua 11 wameuawa katika mji mkuu wa Mali Bamako na makumi ya wengine wamejeruhiwa kufuatia maandamano yanayoendelea yakimtaka Rais wa nchi hiyo Ibrahim Boubacar Keita ajiuzulu.

Maandamano hayo ambayo yameambatana na ghasia kubwa jana yalimlazimisha Rais Keita kuvunja Mahakama ya Katiba ya nchi hiyo, ikiwa ni katika juhudi za kutuliza hali ya mambo, kufuatia maandamano ya ghasia yaliyosababisha shughuli nyingi katika mji mkuu kukwama.

Viongozi wa upinzani nchini Mali wamemtaka Rais Ibrahim Boubacar Keita kujiuzulu, baada ya kukataa makubaliano yaliyolenga kuzuia machafuko yanayoendelea nchini humo.

Siku ya Ijumaa, waandamanaji hao wanaoshinikiza kujiuzulu Rais Keita walijaribu kuyateka majengo kadhaa muhimu ya serikali likiwemo Bunge na jengo la Shirika la Utangazaji la Radio na Televisheni ya nchi hiyo, hali iliyopelekea kuibuka machafuko. Aidha jengo lenye Bunge la nchi hiyo liliharibiwa vibaya baada ya kuvamiwa na waandamanaji hao.

Rais Ibrahim Boubacar Keita

Viongozi wa upinzani wanaounga mkono malalamiko na maandamano hayo walikuwa wamewataka wafuasi wao waanzishe kampeni za uasi wa kiraia na kuyadhibiti majengo muhimu kama ofisi ya Waziri Mkuu ili kumshinikiza Rais Ibrahim Boubacar Keita wa nchi hiyo ajiuzulu.

Wanasema kiongozi huyo ameshindwa kupendekeza mpango muhimu wa kutatua matatizo ya kiusalama na kiuchumi yanayoikabili nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika. Maandamano hayo ni ya tatu makubwa kufanyika katika mji mkuu Bamako katika kipindi cha majuma matatu ya hivi karibuni.

Mgogoro wa kisiasa nchini Mali ambao uliibuka baada ya kufanyika uchaguzi wa Bunge mnamo Machi mwaka huu, umezusha wasiwasi mkubwa si tu ndani ya nchi hiyo, bali pia katika nchi jirani na nchi hiyo.

Tags

Maoni