Jul 27, 2020 13:05 UTC
  • Tundu Antipas Lissu
    Tundu Antipas Lissu

Mwanasheria na mwanasiasa mashuhuri wa kambi ya upinzani nchini Tanzania Tundu Antipas Lissu amewasili nchini humo baada ya kuwa nje ya nchi kwa matibabu kwa zaidi ya miaka miwili, baada ya kunusurika kifo kwa shambulio la risasi akiwa Dodoma.

Lissu ambaye ni Makamu Mwenyekiti Taifa wa chama cha upinzani cha Chadema, amejijengea sifa kama wakili mashuhuri, mwanasiasa shupavu wa upinzani na mkosoaji mkuu wa serikali, na kutokana na makabiliano yake na serikali ya Rais John Magufuli.

Lissu alipigwa risasi akiwa nyumbani kwake mjini Dodoma na kujeruhiwa vibaya Septemba 7, 2017, na watu wasiojulikana.

Siku chache kabla ya kurejea nchini Tanzania mwanasiasa huyo wa kambi ya upinzani aliyekuwa mbunge wa jimbo la Singida Mashariki, alisema kuwa anarudi nchini katika mazingira ambayo hatari dhidi yake bado haijaondoka.

''Wale waliokuja kuniua hiyo siku ya tarehe saba Septemba miaka mitatu iliyopita na waliowatuma au waliowalipa au waliowaelekeza bado wanaitwa watu wasiojulikana, maana yake ni kwamba hao watu bado wapo na kwa sababu bado wapo na hawajasema kama lengo lao la kuniua wameliacha, bado kuna hatari juu ya maisha yangu'', akisema Tundu Lissu.

Tundu Lissu

Lissu alijipatia umaarufu mkubwa baada ya kuwa mtetezi wa haki za wachimbaji wadogo na wananchi wanaoishi katika maeneo ambako kampuni kubwa za uchimbaji madini zilikuwa zimepewa leseni za uchimbaji kutokana na mabadiliko ya kisera yaliyofanywa na utawala wa rais mstaafu wa Tanzania Benjamin Mkapa aliyeaga dunia siku chache zilizopita.

Kilele chake kilikuwa suala la mgodi wa Bulyanhulu ambako Lissu na wanaharakati wengine walidai kuwa kulikuwa na wachimbaji wadogo waliofukiwa ardhini ili kupisha uchimbaji wa kampuni kubwa kutoka nje ya nchi.

Tags