Aug 03, 2020 07:37 UTC
  • Jeshi la Libya: Russia inatuma silaha huko Libya

Jeshi la Serikali ya Mwafaka wa Kitaifa ya Libya limedai kuwa Russia inatuma wanajeshi na zana za kijeshi katika kituo cha jeshi la anga cha al Jufra nchini Libya.

Abdulhadi Dirah Msemaji wa kikosi cha oparesheni cha pamoja katika jeshi la Libya huko Sirte na Jufra ameeleza kuwa: Russia siku chache zilizopita ilituma ndege kadhaa za kijeshi zenye zana na silaha katika moja ya vituo vya anga huko Libya. Abdulhadi Dirah ameongeza kuwa ndege tano za kijeshi aina ya Ilyushin zimetua katika kituo cha jeshi la anga cha al Jufra katikati ya Libya.  

Abdulhadi Dirah, Msemaji wa kikosi cha oparesheni za pamoja cha jesh la Libya huko Sirte na Jufra 

Aidha amesema kuwa, ndege nne za mizigo za Russia zimetua katika mji wa Benghazi na katika uwanja wa ndege wa al Abraq katikati ya Libya; na kwamba ndege hizo zilikuwa zimewabeba mamluki. 

Kwa sasa Libya ina serikali mbili; moja ikiwa ile inayotambuliwa rasmi na Umoja wa Mataifa yenye makao makuu huko Tripoli, mji mkuu wa Libya chini ya uongozi wa Waziri Mkuu, Fayez al Sarraj, na serikali nyingine ina makao yake katika mji wa Tobruk mashariki mwa nchi, inayoungwa mkono na Imarati, Misri, Saudi Arabia na nchi kadhaa za Ulaya.  

Uturuki pia inaiunga mkono Serikali ya Mwafaka wa Kitaifa ya Libya.

Tags

Maoni