Aug 03, 2020 09:27 UTC
  • NEC: Uchaguzi Mkuu wa Tanzania kugharimu shilingi bilioni 331

Tume ya Taifa ya Uchaguzi ya Tanzania (NEC) inatarajia kutumia shilingi bilioni 331.7 kukamilisha zoezi la Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Oktoba 28, mwaka huu ambapo fedha hizo zitatolewa na Serikali.

Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Tanzania (NEC), Jaji Mstaafu, Semistocles Kaijage amesema kuwa, fedha hizo zitatolewa kupitia Mfuko Mkuu wa Hazina kwa kuzingatia kifungu cha 122 cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi, hatua iliyopongezwa kwa serikali kugharamia uchaguzi huo.

Jaji Kaijage ameongeza kuwa, jumla ya wapiga kura milioni 29.2 wamejiandikisha kupiga kura za madiwani, wawakilishi, wabunge na Rais.

Aidha amesema kutokana na idadi hiyo ya wapiga kura, kutakuwa na vituo 80,155 vya kupigia kura na kila kituo kimoja kitahudumia wapiga kura wasiozidi 500.

Freeman Mbowe, kiongozi wa chama kikuu cha upinzani cha  Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA)

Kwa mujibu wa NEC uchaguzi mkuu wa Tanzania utafanyika Jumatano ya Oktoba 28 mwaka huu, huku kampeni zikitarajiwa kuanza August 26 hadi Oktoba 27, 2020.

Licha ya kupongezwa kwa hatua mbalimbali za maendeleo zilizochukuliwa na serikali yake, zikiwemo za kustawisha miundomsingi ya kiuchumi na kupambana na ufisadi, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, John Pombe Magufuli amekuwa akikosolewa kwa madai kuwa anaminya na kukandamiza demokrasia sambamba na kuendesha kampeni ya kuua vyama vya upinzani katika nchi hiyo ya Afrika Mashariki.

Wanasiasa wa upinzani wanadai kuwa serikali ya sasa ya Rais Magufuli imeweka mazingira magumu ya kufanya mikutano ya kisiasa na hivyo kukandamiza demokrasia. Hata hivyo serikali ya Magufuli inakanusha madai hayo ikisisitiza juu ya umuhimu wa kuheshimiwa sheria na kujiepusha na vitendo vya uchochezi kwa kisingizio cha demorasia.

Maoni