Aug 05, 2020 10:56 UTC
  • Kenya yaanzisha uchunguzi baada ya helikopta yake ya kijeshi kuanguka Somalia

Jeshi la Ulinzi la Kenya (KDF) limeanzisha uchunguzi baada ya helikopta yake kuanguka kusini mwa Somalia, na kusababisha wanajeshi wake 10 kujeruhiwa.

Msemaji wa Jeshi la Ulinzi la Kenya Bi. Zipporah Kioko amesema helikopta hiyo ilikuwa kwenye safari zake za kawaida wakati iilipoanguka Jumatatu jioni  kwenye uwanja wa Dhobley. Amesema wanajeshi wote 10 waliokuwa kwenye helikopta hiyo sasa wako kwenye hospitali ya jeshi mjini Nairobi wakiendelea vizuri.

Habari zinasema helikopta hiyo ilikuwa njiani kurudi baada ya kusafirisha mahitaji kwa wanajeshi wa Kenya ambao ni sehemu ya wanajeshi 4,000 wa kikosi cha tume ya Umoja wa Afrika nchini Somalia AMISOM walioko kwenye eneo la Lower Juba kwenye mpaka na Kenya.

Askari wa AMISOM nchini Somalia

Hii ni mara ya tatu kwa ajali ya ndege inayoihusisha Kenya kutokea nchini Somalia mwaka huu, ya kwanza ilikuwa ni ile ndege iliyokuwa imebeba vifaa vya kukabiliana na corona iliyotunguliwa kwa makosa na wanajeshi wa Ethiopia na kuwaua watu sita, na nyingine ya kiraia ya iliyoanguka tarehe 14 Julai wakati inatua katika mji wa Beledweyne katika eneo la Hiiran kusini mwa Somalia.

Askari wapatao 21,000 wa Amisom hawajaweza kurejesha uthabiti na usalama kamili nchini humo hasa katika mji mkuu Mogadishu.

Tags

Maoni