Aug 09, 2020 08:13 UTC
  • Ethiopia yatishia kuvunja uhusiano na Marekani, yasema Washington ndio itayopata hasara

Ethiopia imetishia kuvunja uhusiano wake wa kidiplomasia na Marekani kufuatia uingiliaji kati wa Washington katika kadhia ya Bwawa la Renaissance la Addis Ababa.

Katika jibu dhidi ya mashinikizo ya Marekani ya kuitaka Addis Ababa isaini mkataba wa makubaliano na Misri na Sudan kuhusiana na bwawa hilo, msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Ethiopia Dina Mufti amesema: Katika kulinda maslahi yake, Ethiopia haitasalimu amri kwa mashinikizo ya Marekani; na mashinikizo hayo yanaweza kupelekea kuvunjwa uhusiano wa Addis Ababa na Washington. Amesisitiza kuwa Ethiopia haitapata hasara kwa kuvunjika uhusiano huo, bali ni Marekani ndiyo itakayopata hasara.

Mufti amesema, hakuna shinikizo lolote litakaloizua Ethiopia kukamilisha ujenzi wa bwawa la Renaissance. Amefafanua kuwa Addis Ababa haiwezi kusaini mkataba wa makubaliano unaoainisha mgao maalumu wa maji ya bwawa la Renaissance kwa nchi mbili za Misri na Sudan.

Bwawa la Renaissance

Katika kikao cha wiki iliyopita cha mawaziri wa maji na nishati wa Ethiopia, Misri na Sudan cha kujadili ujazaji maji ya Mto Nile katika bwawa la Renaisssance, Addis Ababa iliwatangazia Cairo na Khartoum kuwa endapo utatokea ukame, itazingatia hali za nchi hizo ili kuziwezesha kukikabili na kukivuka kipindi cha janga hilo.

Kwa mujibu wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Ethiopia kikao kingine cha  mazungumzo ya pande hizo tatu kitafanyika kesho Jumatatu.../

Tags

Maoni