Aug 09, 2020 11:48 UTC
  • Rais wa Chad: Boko Haram wataendelea kuvuruga usalama kwa muda mrefu licha ya operesheni kubwa dhidi yao

Rais Idriss Deby wa Chad amesema kuwa, kundi la kigaidi la Boko Haram litaendelea kuvuruga amani na usalama kwa muda mrefu katika eneo la Ziwa Chad licha ya kuanzishwa operesheni kubwa dhidi ya kundi hilo mapema mwaka huu.

Rais wa Chad amesema hayo katika mahojiano yake na vyombo vya habari na kusisitiza kwamba, tutaendelea kushuhudia harakati za kuvuruga amani na usalama za Boko Haram kwa muda mrefu katika eneo la Ziwa Chad.

Wanamgambo wa Boko Haram walianzisha mashambulizi nchini Nigeria mwaka 2009, na  2015 kundi hilo la kigaidi lilipanua mashambulio yake hadi katika nchi jirani za Niger, Cameroon na Chad.

Nchi zinazopakana na Ziwa Chad yaani Nigeria, Chad, Niger na Cameroon zimeanzisha kikosi cha pamoja cha kukabiliana na wanamgambo wa Boko Haram ambao hadi sasa wameshasababisha maafa makubwa ya roho za watu, mali za umma na kukwamisha maendeleo ya nchi za eneo hilo. Nchi ya Benin nayo hivi karibuni ilitangaza kujiunga na kikosi hicho. Hata hivyo inaonekana kuwa, kikosi hicho kimeshindwa kulitokomeza kundi hilo la Boko Haram.

Wapiganaji wa kundi la kigaidi la Boko Haram

Zaidi ya watu elfu 30 wameuawa na wengine wanaokaribia milioni tatu wamelazimishwa kuwa wakimbizi kutokana na mashambulizi ya kundi hilo la Boko Haram nchini Nigeria tokea mwaka 2009.

Maeneo ya kaskazini mashariki mwa Nigeria ambayo yanahesabiwa kuwa ngome ya wanamgambo hao wa kundi la Boko Haram yanakabiliwa na hali mbaya ya kibinadamu.

Maoni