Aug 10, 2020 09:50 UTC
  • Machafuko yatanda katika mji wa Port Sudan kutokana na hitilafu za kikabila

Gavana wa jimbo la Bahrul Ahmar nchini Sudan amepiga marufuku watu kutembea katika baadhi ya mji wa Port Sudan ambao ni wa pili kwa ukubwa nchini Sudan kutokana na ghasia zilizotokana na hitilafu za kikabila ambazo zimesababisha mauaji ya watu kadhaa na kujeruhi makumi ya wengine.

Marufuku hiyo ya kutoka nje inawazuia wakazi wa mji wa Port Sudan kutembea nje kuanzia saa 11 jioni hadi saa 12 asubuhi.

Gavana wa jimbo hilo amewataka askari usalama kutumia risasi hai iwapo italazimu kwa ajili ya kutuliza machafuko hayo ambayo yametokea baina ya raia wa makabila ya Nuba na Bani Amer.  

Tume Kuu ya Madaktari wa Sudan imetangaza kuwa, machafuko yaliyotokea baina ya watu wa makabila hayo mawili yamesababisha vifo vya watu wasiopungua wanne na kujeruhi wengine 35.

Port Sudan

Watu walioshuhudia wanasema kuwa machafuko yalianza wakati watu wa kabila la Nuba walipokuwa wakirejea makwao baada ya maandamano dhidi ya mtawala mpya wa mji huo.

Ripoti zinasema kuwa, waandamanaji hao walipita katika maeneo ya makazi ya watu wa kabila la Bani Amer ambao walidhani kwamba wamehujumiwa na mahasimu wao. Mwezi Januari mwaka huu pia watu 9 waliuawa katika mapigano ya kikabila baina ya watu wa makabila hayo na wengine 60 walijeruhiwa.

Watu wa makabila hayo mawili wanaishi katika vitongoji vya watu maskini zaidi katika mji wa Port Sudan wenye bandari kubwa zaidi ya kuingiza na kusafirisha nje bidhaa kupitia Bahari Nyekundu.

Tags