Aug 12, 2020 10:54 UTC
  • Simu zenye kipimajoto zatengenezwa Uganda kusaidia vita dhidi ya corona

Kampuni moja ya China iliyoko nchini Uganda imeanza kutengeneza simu za kisasa za mkononi (smartphone) zenye uwezo wa kupima joto la mwili.

Kampuni ya ENGO  iliyoko wilaya ya Mukono imetangaza kuwa, uvumbuzi huo ni muhimu kwa biashara baada ya miezi minne ya kufungwa kwa shughuli za biashara nchini Uganda.

Katibu wa mkurugenzi mkuu wa kampuni hiyo David Beecham Okwere amesema, utengenezaji wa simu hiyo umetumia kipindi cha miezi minne kwa kuungwa mkono na kampuni mama iliyoko China.

Ameongeza kuwa simu hiyo kwa sasa inafanyiwa mchakato wa ukaguzi wa viwango na Mamlaka ya Viwango nchini Uganda, na kuongeza kuwa majaribio ya awali yameonyesha kuwa simu hiyo inaweza kupima joto la mwili kwa usahihi bila kuwa na muda wa kusubiri.

Kiwanda cha simu cha ENGO nchini Uganda

Waziri wa nchi anayeshughulikia uwekezaji wa Uganda Evelyn Anite amesema, maendeleo hayo ni habari njema kwa Uganda na Afrika, hususan wakati huu ambapo maambukizi ya virusi vya Corona yanaongezeka.

Kwa mujibu wa Okwere simu hiyo itagharimu karibu dola 100 na hivyo watu wengi vijijini Uganda yamkini wasiweze kumudu kuinunua hivyo amesema serikali inapaswa kutoa ruzuku ili iweze kuuzwa kwa bei nafuu. Anite amesema yamkini serikali iondoe ushuru na vishawishi vingine ili simu hiyo iuuzwe kwa bei nafuu.

Hadi kufikia Agosti 11, Uganda ilikuwa na kesi 1,313 za corona huku watu tisa wakiwa wameaga dunia kutokana na ugonjwa huo.

 

Tags

Maoni