Aug 12, 2020 10:58 UTC
  • Watu 19 wauawa katika jaribio la magaidi wa Al Shabab kutoroka gerezani Mogadishu

Watu 19 wameuawa wakati wafungwa ambao ni wafuasi wa kundi la kigaidi wa Al Shabab walipojaribu kutoroka katika gereza moja katika mji mkuu wa Somalia, Mogadishu.

Taarifa zinasema wafungwa 15 na askari 4 waliuawa katika majibizano ya risasi gerezani mjini Mogadishu, wakati wafungwa ambao ni wafuasi wa Al Shabab walipowafyatulia risasi walinzi wa gereza baada ya kujaribu kutoroka kutoka gereza hilo katika mji mkuu wa Somalia, Mogadishu.

Jeshi la Magereza la Somalia  limethibitisha kujiri tukio hilo siku ya Jumatatu na kusema ufatulianaji huyo wa risasi ulisababisha vifo vya watu 19 na wengine 8 kujeruhiwa.

Baadhi ya duru zinasema milipuko ya maguruneti ilisikika karibu na jela hiyo na kwamba silaha hizo ziliingizwa katika jela hilo siku za hivi karibuni.

Serikali ya Somalia imeanza kuchunguza tukio hilo hasa jinsi wafungwa hao walivyopata silaha. Imedokezwa kuwa wafungwa wote waliokuwa na silaha waliuawa.

Tokea mwaka 2008, magaidi wa Al Shabab wamekuwa wakiendesha kampeni ya kutaka kuipindua serikali ya Somalia inayotambuliwa kimataifa. Magaidi hao walitimuliwa kutoka mji mkuu wa Somalia, Mogadishu mwaka 2008 kufuatia oparesheni ya vikosi vya kulinda amani vya Umoja wa Afrika kwa ushirikiano na Jeshi la Somalia lakini bado magaidi hao wanaendelea kutekeleza mashambulizi ya kuvizia mjini humo.

 

 

Tags