Aug 13, 2020 08:11 UTC
  • Wanamgambo wenye mfungamano na Daesh waiteka bandari muhimu nchini Msumbiji

Vyombo vya usalama nchini Msumbiji vimetangaza kuwa, wapiganaji wa kundi lenye mfungamano na kundi la kigaidi la Daesh wameiteka na kuidhibiti bandari moja muhimu kaskazini mwa nchi hiyo.

Kwa mujibu wa vyombo vya usalama wapiganaji wa kundi hilo la kigaidi jana walifanikiwa kudhibiti bandari muhimu yenye utajiri wa gesi katika mji wa Mocimboa da Praia uliopo kaskazini mwa nchi hiyo.

Taarifa zaidi zinasema kuwa, wanamgambo hao ambao wanajiita  Ahlu Sunnah Wa-Jamaa wamefanikiwa kuidhibiti bandari hiyo yenye utajiri baada ya mapigano na mashambulio ya wiki kadhaa baina yao na vikosi vya serikali.

Wakati huo huo vikosi vya ulinzi na usalama vya Msumbiji (FDS) vimetangaza kuwa, vimewaua magaidi 59 katika wiki za hivi karibuni katika jimbo la kaskazini la Cabo Delgado kufuatia operesheni za vikosi hivyo dhidi ya wanamgambo wa  Ahlu Sunnah Wa-Jamaa.

Rais Filipe Nyusi wa Msumbiji ambaye serikali yake inakabiliwa na changamoto kkubwa ya ukosefu wa usalama kaskazini mwa nchi hiyo

Uasi wa wanamgambo nchini Msumbiji umeibuka na kuwa vita vya wazi katika miaka ya hivi karibuni, huku kukiwa na ripoti za mauaji, watu kukatwa vichwa na kutekwa kwa miji miwili katika mkoa wa kaskazini wa Cabo Delgado.

Vijiji vya mkoa huo wa Cabo Delgado ulioko kaskazini mwa Msumbiji tangu mwezi Oktoba mwaka 2017 vimekuwa vikishuhudia mashambulizi ya umwagaji damu ya wanachama wa kundi linalojiita Ahlu Sunna Wal Jamaa, ambao wakazi wa maeneo hayo wanawatambua kwa jina la al-Shaabab.

Kundi hilo la kigaidi limekuwa likifanya mashambulizi hayo licha ya serikali ya Msumbiji kutuma wanajeshi na polisi katika maeneo hayo ambayo yapo katika mpaka wa nchi hiyo na Tanzania