Aug 13, 2020 08:12 UTC
  • TMA: Hakuna tishio la kutokea mawimbi ya tsunami Tanzania

Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imetangaza kuwa, hakuna tishio la kutokea kwa mawimbi makubwa ya tsunami nchini humo kufuatia tetemeko la ardhi la jana usiku.

Kutokana na tetemeko hilo kutokea baharini, kumekuwa na hofu kuwa linaweza kusababisha mawimbi makubwa ya tsunami. Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania imefanya uchambuzi wa taarifa za tetemeko hilo katika kituo chake cha tahadhari ya tsunami ili kuona iwapo kuna uwezekano wowote wa tetemeko hilo kusababisha mawimbi ya tsunami baharini. Matokeo ya uchambuzi huo yanaonesha kuwa, hakuna tishio la tsunami kutokana na tetemeko hilo,” imeeleza taarifa ya TMA.

Kwa mujibu wa TMA tetemeko hilo halikuwa na nguvu kubwa na hakuna maporomoko ya ardhi yaliyojitokeza baharini ambayo yangeweza kuzalisha tsunami. Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania imewataka watumiaji wa eneo la bahari ikiwa ni pamoja wananchi wanaoishi katika maeneo yaliyokaribu na Bahari ya Hindi kutokuwa na hofu na kuendelea na shughuli zao kama kawaida kwa kuzingatia taarifa ya hali ya hewa baharini kama ilivyotolewa awali na Mamlaka.”

Tetemeko a ardhi lililotokea jana 12/08/2020 nchini Tanzania

Tetemeko kubwa la ardhi lenye ukubwa wa 6.0 katika kipimo cha rishta  liliitikisa Tanzania jana usiku, hasa jiji la Dar es Salaam na maeneo ya Mkoa wa Pwani na Zanzibar na kuibua wasiwasi na taharuki miongoni mwa wananchi. Taarifa zinasema tetemeko hilo lilitokea majira ya  saa 2:13  usiku na lilihisika pia katika nchi jirani ya Kenya.

Kwa mujibu wa tovuti ya volcanodiscovery, kitovu cha tetemeko hilo kilikuwa kilomita 82 kusini mashariki mwa Dar es Salaam katika Bahari ya Hindi na kina chake kilikuwa ni takribani kilomita 25.

Maoni