Aug 13, 2020 14:09 UTC
  • Ethiopia yaionya Misri kuhusu mpango wake wa kuanzisha kituo cha kijeshi Afrika Mashariki

Ethiopia imetoa onyo kuhusu uamuzi iliochukua Misri wa kutaka kuanzisha kituo cha kijeshi katika eneo la Afrika Mashariki.

Onyo hilo la Ethiopia limetolewa kufuatia mazungumzo ya Rais Abdel Fattah el Sisi wa Misri na Rais Mohamed Abdullahi Mohamed Farmaajo wa Somalia. 

Serikali ya Addis Ababa imesema, uamuzi huo wa Cairo unazusha wasiwasi na utavuruga uthabiti.

Chombo kimoja cha habari cha Kenya kimeripoti kuwa, katika mkutano uliofanyika baina ya marais wa Misri na Somalia, wawili hao walizungumzia mpango wa kuanzisha kituo cha kijeshi katika eneo lililojitangazia mamlaka ya utawala la Jamhuri ya Somaliland.

Hata hivyo kufuatia kutangazwa habari hiyo, afisa mmoja wa serikali ya Misri amesema, lengo la Ethiopia ni kutaka kuichochea jamii ya kimataifa na nchi za mashariki mwa Afrika dhidi ya Cairo.

Afisa huyo wa serikali ya Misri amekanusha pia kuwepo mpango wa kuanzishwa kituo cha kijeshi cha nchi yake katika eneo la Somaliland, akisisitiza kuwa madai yaliyotolewa na viongozi wa Ethiopia si sahihi na hayana ukweli.

Eneo la Jamhuri ya Somaliland ambalo mji mkuu wake ni Hargeisa, lilitangaza kujitenga na Somalia mwaka 1991 na kujiundia utawala wake ambao hata hivyo haujatambuliwa rasmi na nchi yoyote duniani.

Inafaa kukumbusha kuwa uhusiano wa Misri na Ethiopia umekuwa wa vuta nikuvute kutokana na masuala kadhaa likiwemo la mzozo juu ya mgao wa maji ya Mto Nile na ujazaji maji ya mto huo kwenye Bwawa la An-Nahdhah au Renaissance lililojengwa na Ethiopia.../

Tags