Aug 14, 2020 08:02 UTC
  • Mashirika ya petroli DRC yasimamisha mgomo baada ya mapatano

Mashirika yanayouza mafuta ya petroli katika maeneo ya kusini na mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo yamesitisha mgomo wa siku kadhaa, baada ya serikali kuafiki kuongeza bei ya bidhaa hiyo.

Serkali ya DRC imetoa jibu kwa matakwa yao na sasa bei ya lita moja ya petroli imepanda kwa kiwango cha asilimia 24, jambo ambalo litawaumiza wananchi wa kawaida.

Mazungumzo kati ya Waziri Mkuu Sylvestre Ilunga Ilunkamba na ujumbe wa wafanyabiashara katika sekta ya mafuta yalidumu siku mbili jijini Kinshasa.

Albert Yuma kiongozi wa muungano wa vyama vya wafanyabiashara amesema mgomo hausaidii chochote, bali umepelekea uchumi kudidimia. Pande zote mbili zimefikia makubaliano hasa kuhusu bei ya petroli.

Waziri wa Uchumi Acacia Bandubola  alitangaza Alhamisi kuwa sasa lita moja ya mafuta itauzwa kwa senti 96 badala ya 73, bei iliyokuwa ikiuzwa hapo  awali.

Mashirika ya mafuta yanasema yamekuwa yakipata hasara kutokana na kuporomoka thamani ya franga ya Congo. Mashirika hayo yanasema yananunua mafuta kwa sarafu ya dola na kuuza kwa faranga na hivyo kupata hasara kwa kuzingatia kuwa bei inadhibitiwa na serikali.

 

Tags

Maoni