Aug 18, 2020 13:38 UTC
  • Ripoti za jaribio la mapinduzi Mali, milio ya risasi yasikika Bamako, na mawaziri watiwa nguvuni

Jeshi la Mali limeweka vizuizi katika kambi moja iliyopo katika viunga vya mji mkuu wa nchi hiyo, Bamako huku raia wa eneo hilo wakisema kuwa milio ya risasi inaendelea kusikika katika eneo hilo.

Ripoti za watu walioshuhudia zinasema wanajeshi waliokuwa na hasira waliondoka katika kambi hiyo wakiwa kwenye magari ya kijeshi na kuwatia nguvuni mawaziri wa mambo ya nje na fedha na vilevile Spika wa Bunge la Mali.

Shirika la habari la AFP limewanukuu watu walioshuhudia wakisema kuwa, mapema leo wanajeshi wa Mali walikuwa wakifyatua risasi angani kwa sababu zisizojulikana katika kambi kubwa ya jeshi ya Kati iliyoko umbali wa kilomita 9 kutoka Bamako.

Daktari wa hospitali moja ya eneo la Kati amenukuliwa akisema milio ya risasi ilikuwa ikisikika mapema leo katika kambi ya jeshi ya Kati.

Jarida la Jeune Afrique linalojihusisha na masuala ya Afrika limeripoti kuwa ufyatuaji risasi huo ni sehemu ya mapinduzi ya kijeshi dhidi ya Rais wa Mali.

Ripoti ya jarida hilo imesema kuwa milio mingine ya risasi imesikika kandokando ya makazi ya Waziri Mkuu wa Mali, Boubou Cissé.

Maandamano ya wapinzani wa serikali mjini Bamako

Duru za habari zinasema kunashuhudiwa uasi wa kijeshi nchini Mali huku vikosi vya askari wa nchi hiyo vikielekea Bamako.

Mali inasumbuliwa na machafuko ya kisiasa kwa kipindi cha miezi miwili sasa. Maelfu ya wafuasi wa kambi ya upinzani wamekuwa wakifanya maandamano nchini humo wakimtaka Rais Ibrahim Boubacar Keita na Waziri Mkuu wake, Boubou Cissé wajiuzulu.

Tags