Sep 06, 2020 02:27 UTC
  • Mazungumzo baina ya pande hasimu nchini Libya yameanza huko Morocco

Mazungumzo baina ya pande mbili hasimu nchini Libya yalianza jana Jumamosi katika viunga vya mji mkuu wa Moroco Rabat.

Mazungumzo hayo yanayofanyika kwa kiwango cha wataalamu yaanatarajiwa kuendelea hadi kesho Jumatatu. Mwaka 2015 mji wa Skhirat wa Morocco ulikuwa mwenyeji wa mazungumzo ya amani ya Livya ambapo pande mbili zilitiliana saini makubaliano kwa usimamizi wa Umoja wa Mataifa na wawakilishi kadhaa kutoka nchi za Kiarabu na Magharibi.

Ijapokuwa serikali ya Mwafaka wa Kitaifa ya Libya iliundwa mwaka 2015 kwa mujibu wa makubaliano na kwa usimamizi wa Umoja wa Mataifa, vikosi vitiifu kwa jenerali muasi Khalifa Haftar anayeungwa mkono na bunge la serikali ya Tabrook havikuitambua serikali hiyo; na kuanzia Aprili 4 mwaka uliopita wa 2019 vilianzisha operesheni za mashambulio kwa lengo la kuuvamia na kuukalia mji mkuu wa Libya, Tripoli.

Machafuko nchini Libya yamevuruga kabisa maisha ya wananchi wa nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika

Hatua hiyo ya wanamgambo watiifu kwa Haftar imegonga mwamba hadi sasa kutokana na jibu la vikosi vya serikali ya Mwafaka wa Kitaifa, lakini imezidi kuvuruga amani na uthabiti katika nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika.

Libya ilitumbukia katika machafuko na vita vya ndani baada ya wanajeshi wa Marekani wakishirikiana na wale wa Shirika la Kijeshi la Nchi za Magharibi (NATO) kuishambulia nchi hiyo na kusaidia harakati za kumuondoa madarakani aliyekuwa kiongozi wa nchi hiyo Kanali Muammar Gaddafi hapo mwaka 2011.

Tags