Sep 16, 2020 11:14 UTC
  • Tanzania yaondoa marufuku ya ndege za Kenya; baada ya wanaotoka Tanzania kutokaa karantini

Tanzania imetangaza kuondoa marufuku ya safari za ndege za Kenya iliyokuwa imeiweka mwezi uliopita, kulingana na taarifa ya Mamlaka ya safari za anga nchini Tanzania TCAA.

Tanzania ilikuwa imeziwekea marufuku ndege za Kenya Airways, Fly 54, Safarilink na AirKenya express kama hatua ya kujibu hatua ya karantini iliyowekwa awali na Kenya. Hata hivyo ndege hizo sasa zitaruhusiwa kufanya safari zake nchini Tanzania.

Kenya ilisema ilichukua hatua ya kuwaweka baadhi ya wasafiri karantini baada ya kuwasili nchini humo wakiwemo wale wanaotoka nchini Tanzania, kama njia mojawapo ya upunguzaji wa kusambaa kwa virusi vya corona.

Hatua hiyo ya Tanzania inakuja baada ya Kenya kuondoa sharti la kuwaweka karantini kwa muda wa siku 14 Watanzania wanoingia nchini humo.

Hatua zilizochukuliwa na nchi hizi mbili jirani zilizuwia usafiri wa anga baina yake zilitia dosari mahusiano yake ya kidiplomasia na hata kuelezwa kuwa, kuna mzozo na mgogoro wa chini kwa chini baina ya nchi hizo.

Baada ya miezi kadhaa ya mvutano kuhusu namna nchi hizo mbili zinavyoshughulikia janga la corona, sasa mambo yanaonekana kupoa.

Kwa muda sasa serikali ya Kenya ilikuwa inahofia kuwa Tanzania haiko wazi kuhusu namna inavyoshughulikia janga la corona hatua mabayo pia imewahi kukoselewa na asasi za kimataifa.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania John Pombe Magufuli alitangaza kuwa ugonjwa huo umekwisha nchini humo na hivi sasa kuvaa barakoa na kutochangayikana watu suala nadra nchini Tanzania.

Maoni