Sep 16, 2020 11:15 UTC
  • Burundi yataka kurejesha uhusiano wake na Umoja wa Mataifa

Serikali ya Burundi imetangaza kuwa, inataka kurejesha uhusiano wake na Umoja wa Mataifa ambao ulizorota katika kipindi cha utawala wa aliyekuwa Rais wa nchi hiyo Pierre Nkurunziza.

Taarifa ya serikali ya Burundi imesema kuwa, nchi hiyo inataka ushirikiano utakaojikita hasa katika sekta ya kijamii na kiuchumi, kulingana na "Mpango wa Maendeleo wa Kitaifa".

Baada ya kuingia madarakani Rais Evariste Ndayishimiye ambaye ni jenerali mstaafu hali inaonekana kubadilika katika sera na siasa za nchi hiyo.

Wakati huo huo ujumbe wa ngazi ya juu wa Umoja wa Mataifa umetumwa nchini Burundi kutathmini hali halisi ya mambo katika nyanja za kijamii na kiuchumi, kisiasa, kibinadamu na haki za binadamu tangu mwaka 2015. Ujumbe huo utakutana wakati wa ziara hiyo na Rais Ndayishimiye mara mbili, wajumbe wa serikali, chama tawala na upinzani, viongozi wa dini, vyama vya kiraia na mabalozi mbalimbali wa nchi za kigeni nchini Burundi.

Vyombo vya usalama nchini Burundi vinatuhumiwa kukiuka haki za binadamu

 

Serikali ya Burundi chini ya uongozi wa Nkurunziza iliandamwa na tuhuma nyingi za kufanya ukandamizaji mkubwa wa umwagaji wa damu dhidi ya wapinzani katika kona mbalimbali za Burundi. Baadhi ya wachambuzi wa mambo wanalituhumu moja kwa moja tawi la vijana la chama tawala cha CNDD-FDD kuwa ndio wanaohusika na mauaji ya wapinzani.

Hata hivyo serikali ya Burundi imekuwa ikikanusha madai hayo na kueleza kwamba, ni propaganda chafu dhidi ya serikali ya nchi hiyo ambazo zimekuwa zikiendeshwa kwa kutegemea vyanzo visivyo vya kuaminika.

Maoni