Sep 16, 2020 11:19 UTC
  • Tanzania yapinga vikali ripoti ya Umoja wa Mataifa kuhusu haki za binaadamu katika nchi hiyo

Waziri wa Mashauri ya Kigeni na Ushirikiano wa Afrika Mashariki wa Tanzania amepinga vikali ripoti ya Tume ya Haki za Binaadamu ya Umoja wa Mataifa iliyosema kuwa, kumekuwepo hali ya "kuongezeka kwa ukandamizaji wa kidemokrasia na haki za raia nchini humo.

Profesa Palamagamba Kabudi amesema kuwa, tathimini iliyotolewa na Tume ya Haki za Binaadamu ya Umoja wa Mataifa hailingani na uhalisia wa hali ilivyo nchini Tanzania.

Amesema kuwa, tayari wamemtaka balozi wa Tanzania katika ofisi za Umoja wa Mataifa mjini Geneva Uswisi kuwasilisha malalamiko ya kupinga ripoti hiyo ambayo amesema, haina ukweli wowote. Profesa Kabudi amesema kuwa, wakati Tanzania ikijiandaa kwa ajili ya uchaguzi mkuu mwezi ujao wagombea wote wa urais wanafanya kampeni zao kwa uhuru kamili na hakuna mgombea aliyekwamishwa katika kampeni zake. Hata hivyo, waziri huyo hakuashiria mlolongo wa wagombea Ubunge na Udiwani wa upinzani ambao majina yao yamekatwa kwa kile kinachoelezwa na upinzani kuwa, mizengwe na njama za chama tawala za kujiandalia mazingira ya ushindi.

Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa Michelle Bachelet

 

Ikumbwe kuwa, Tume ya Haki za Binaadamu ya Umoja wa Mataifa imetoa taarifa juu ya haki za binaadamu maeneo mbalimbali duniani na kuonesha wasiwasi wake juu ya hali ya haki za binadamu Tanzania. Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa Michelle Bachelet ameeleza katika taarifa hiyo kuwa nchini Tanzania kumekuwepo hali ya "kuongezeka kwa ukandamizaji wa kidemokrasia na haki za raia, hali ambayo inazidi kufanya mazingira ya haki za binadamu kuwa duni.

Kamishna Bachelet amesema wakati uchaguzi ukitarajiwa kufanyika mwezi ujao nchini Tanzania, ''tumekuwa tukipokea ripoti kuhusu ukamataji holela na kushikiliwa kwa wanaharakati, waandishi wa habari na wapinzani.

Maoni