Sep 17, 2020 08:10 UTC
  • Makumi ya wafungwa watoroka jela nchini Uganda

Makumi ya wafungwa wametoroka jela katika wilaya ya Moroto, kaskazini mashariki mwa Uganda na kukimbilia kusikojulikana.

Msemaji wa Idara ya Magereza ya Uganda, Frank Baine amesema wafungwa hao walitoroka jela jana Jumatano, baada ya kadhaa miongoni mwao kuwafyatulia risasi askari waliokuwa wanawalinda.

Amesema, "kumejiri tukio la kutoroka jela. Tungali tunajaribu kukusanya taarifa juu ya tukio hilo sanjari na kuwabaini wafungwa waliotoroka."

Bila kutaja idadi kamili, Msemaji wa Idara ya Magereza ya Uganda amesema idadi ya wafungwa waliokimbia jela ni kubwa mno.

Wafungwa katika Gereza Kuu la Luzira nchini Uganda

Kadhalika ametoa mwito kwa wafungwa hao kujisalimisha kwa taasisi husika na kueleza bayana kuwa, maafisa usalama wakiwemo wanajeshi na askari polisi wanawasaka wafungwa hao ili kuwakamata tena na kuwarudisha jela.

Itakumbukwa kuwa, Machi mwaka huu, wafungwa watatu waliuawa huku wengine sita wakijeruhiwa katika jaribio jingine la kutoroka gerezani katika wilaya ya Arua, kaskazini magharibi mwa Uganda.

 

Tags

Maoni