Sep 18, 2020 02:42 UTC
  • Sisitizo la Umoja wa Mataifa la kutekelezwa vikwazo vya silaha dhidi ya Libya

Hali ya wasiwasi kuhusu mgogoro wa kisiasa unaoikabili Libya na hali inayolegalega nchini humo ni mambo ambayo yangali yanaendelea kushuhudiwa licha ya kutangazwa usitishaji vita nchini humo. Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limepasisha azimio na kutaka kutekelezwa vikwazo vya silaha dhidi ya Libya na kuondolewa mamluki wote katika nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika.

Azimio hilo ambalo limepasishwa kwa kura 13 za ndio huku nchi mbili wanachama wa Baraza la Usalama zikijizuia kupiga kura limetilia mkazo kufanyika mazungumzo ya kisiasa kati ya pande zinahusika na mzozo huo ndani ya Libya na kuheshimiwa kikamilifu usitishaji vita. 

Hali ya kisiasa huko Libya imebadilika katika wiki za hivi karibuni. Baada ya kupamba moto vita kati ya vikosi vya Serikali ya Mwafaka wa Kitaifa ya Libya na  wanamgambo wanaojiita Jeshi la Taifa la Libya chini ya uongozi wa jenerali muasi Khalifa Haftar, pande mbili hizo ziliafiki kusimamisha mapigano; na kusisitiza kuanza tena mazungumzo ili kupatikana njia ya ufumbuzi ya kisiasa kwa ajili ya kuhitimisha mgogoro huko Libya; amapo hadi kufikia sasa kumefanyika vikao kadha wa kadha vya pande mbili na pande kadhaa kati ya viongozi wa Libya na viongozi wa baadhi ya nchi. 

Jenerali muasi, Khalifa Haftar wa nchini Libya

Ukweli wa mambo ni kuwa, pande zinazozozana huko Libya zinafanya juhudi kupitia mazungumzo ziweze kugawana madaraka ya kisiasa nchini humo na kuandaa uwanja wa kufanyika uchaguzi na kuunda serikali kuu itakayojumuisha makundi mbalimbali ya Walibya. Hata hivyo pamoja na juhudi hizo uingiliaji wa nchi ajinabi nchini humo ungali unaendelea.  

Stephen Williams, Mjumbe wa Muda wa Umoja wa Mataifa Katika Masuala ya Libya amekosoa uingiliaji wa nchi ajinabi nchini humo na kusema: watu wa Libya wana hofu kuhusu mustakbali wa nchi yao. Wamechoshwa na vita na wanataka amani.  

Nchi za eneo na baadhi ya nchi za Magharibi zingali zimejipenyeza waziwazi na nyuma ya pazia katika nyuga za kisiasa na kijeshi hulo Libya.  

Ukweli ni kuwa uungaji mkono wa kijeshi wa nchi mbalimbali unazidisha mgogoro huko Libya. Kutumwa makumi ya shehena za silaha na zana za kivita na pia kutumwa wapiganaji nchini humo yote hayo yamepelekea hali ya mgogoro nchini humo kuwa tata zaidi na ni dhahir shahir kwamba, nchi hiyo sasa imekuwa uwanja wa vita vya niaba vya kuwania madaraka baina ya nchi mbalimbali. Hii ni katika hali ambayo Libya kwa miaka kadhaa sasa inakabiliwa na vikwazo vya silaha vya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa; na viongozi wa taasisi hiyo mara kadhaa wametaka kuheshimiwa vikwazo hivyo na kutotumwa silaha wala zana za kijeshi nchini humo. Kama alivyotahadharisha Antonio Guterres Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa huko nyuma kwamba: kuendelea kukiukwa vikwazo vya silaha vilivyowekwa na Baraza la Usalama kutaifanya ngumu zaidi hali ya mambo nchini Libya.  

Antonio Guterres, Katibu Mkuu wa UN  

Kwa mujibu wa ripoti ya wataalamu wa Umoja wa Mataifa; pande nyingine huko Libya na waungaji mkono wa kimataifa zikiwemo nchi za Imarati, Russia na Jordan zinazomuunga mkono jenerali muasi, Khalifa Haftar huku Uturuki na Qatar zikiiunga mkono Serikali ya Mwafaka wa Kitaifa  ya Libya. Zote zinashutumiwa kwa kukiuka vikwazo vya silaha vya Umoja wa Mataifa dhidi ya nchi hiyo tajiri kwa mafuta ya kaskazini mwa Afrika; na vikwazo havijawa na taaathira yoyote.   

Ukweli ni kuwa, nafasi ya jiopolitiki ya Libya na kuwa kwake karibu na Ulaya imeifanya nchi hiyo kutambuliwa kama lango kuu la kuingilia Afrika; na uwepo wa maliasili tajiri na akiba kubwa ya mafuta umezipelekea nchi mbalimbali duniani kutoa zingatio maalumu kwa Libya. Hivi sasa pia hata kama vikwazo vya silaha dhidi ya Libya vimetiliwa mkazo na kusisitizwa pia mchakato wa mazungumzo ili kurejesha amani nchini humo lakini kivitendo nchi zinazoingilia masuala ya Libya haziko tayari kuondoka katika uga wa siasa na katika medani ya kivita nchini humo. Aidha kuendelea kuwepo wanamgambo waliotumwa nchini humo na Uturuki na vile vile wanamgambo mamluki kutoka Sudan na Imarati ambao wanamuunga mkono jenerali muasi Khalifa Haftar na pia hatua ya Imarati ya kutuma ndege zisizo na rubani (droni) ambazo mara kwa mara hufanya mashambulizi katika maeneo malimbali huko Libya ni ishara ya kutokuwa na athari vikwazo hivyo vya silaha dhidi ya Libya.  

Mamluki wa Sudan wanaopigana huko Libya 

Dakta Ahmad Bakhshi mchambuzi wa masuala ya kisiasa anazungumzia suala hilo akisema, usitishaji vita hauna mwelekeo chanya na hatuwezi kutarajia kumalizika vita na machafuko kupitia suala hilo huko Libya.  

Mazungumzo kwa ajili ya kuiondoa Libya katika mgogoro wa hivi sasa yataendelea lakini hakuna dhamana yoyote iwapo mazungumzo hayo yatakuwa na natija kwa sababu Libya ingali inakabiliwa na uingiliaji wa nchi ajinabi na huku nchi hizo zikiendelea kuziunga mkono kijeshi na kisilaha pande hasimu nchini humo. 

Tags

Maoni