Sep 18, 2020 03:36 UTC
  • Afrika Kusini: Madai ya Marekani dhidi ya Iran ni ya kustaajabisha

Waziri wa Mambo ya Nje wa Afrika Kusini ameeleza juu ya kustaajabishwa na kushangazwa kwake na madai ya Marekani kuwa Iran inapanga kumuua Lana Marks, Balozi wa Marekani nchini Afrika Kusini.

Katika mahojiano na Shirika la Taifa la Utangazaji la Afrika Kusini (SABC News), Dakta Naledi Pandor amesema kuwa, "tumestaajabishwa na kitendo cha kutolewa taarifa kama hiyo kwa umma. Imetushangaza namna ilivyowashangaza pia mafariki zetu nchini Iran."

Waziri wa Ushirikiano na Uhusiano wa Kimataifa wa Afrika Kusini amehoji, "inawezekanaje Iran, rafiki mkubwa wa Afrika Kusini ije hapa nchini na kufanya kitendo kiovu kama hicho katika nchi ambayo pia rafiki yake? Naweza kusema kuwa madai hayo ni ya kushangaza. Sisemi zaidi!"

Mwanadiplomasia huyo wa ngazi za juu wa Afrika Kusini amesema hayo siku chache kabla ya kuanza Mkutano wa Ngazi ya Juu wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mjini New York nchini Marekani kuanzia Jumatatu ijayo ambapo amebainisha kuwa, Afrika Kusini kupitia Wizara ya Usalama wa Taifa, Ayanda Dlodlo imeihakikishia Washington kuwa wanadiplomasia wote wapo salama katika nchi hiyo na kwamba iwapo patahitajika kuchukuliwa hatua za ziada, nchi hiyo haitasita kufanya hivyo.

Jumatatu iliyopita pia, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Afrika Kusini, Lunga Ngqengelele aliyataja madai hayo ya kipropaganda yaliyotolewa na viongozi wa Marekani dhidi ya Iran kuwa hayana msingi wowote.

Kuimarika uhusiano wa Iran na Afrika Kusini licha ya propaganda za maadui

Hii ni baada ya tovuti ya POLITICO kunukuu ripoti za kiintelijensia za Marekani na maafisa walio karibu na serikali ya nchi hiyo na kudai kuwa Iran inapanga kumuua Lana Marks, Balozi wa Marekani nchini Afrika Kusini, eti kama kisasi cha mauaji ya Luteni Jenerali Qassem Soleimani, aliyekuwa Kamanda wa Kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (RGC), ambaye aliuawa shahidi mapema mwaka huu katika shambulizi la kigaidi la jeshi katili Marekani nchini Iraq.

Kadhalika msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran, Sayyid Khatibzadeh amepinga tuhuma hizo za kichochezi na zinazotolewa kwa malengo maalumu dhidi ya Iran, zilizochapishwa na katika vyombo vya habari vya Marekani, ambapo amewataka viongozi wa Marekani waache kutumia mbinu chafu za kukaririwa kwa shabaha ya kueneza proganda chafu dhidi ya Iran kimataifa. Ameongeza kuwa, Iran ikiwa ni nchi mwanachama inayowajibika  katika jamii ya kimataifa, imethibitisha kuheshimu kwake sheria na kanuni za kidiplomasia za kimataifa. 

Tags

Maoni