Sep 18, 2020 08:06 UTC
  • Rais wa Somalia amteua Waziri Mkuu mpya baada ya miezi miwili

Rais Mohamed Abdullahi Mohamed Farmajo wa Somalia amemteua Mohamed Hussein Roble kuwa Waziri Mkuu mpya wa nchi hiyo ya Pembe ya Afrika.

Roble ambaye ni mgeni katika siasa za Somalia amekuja kurithi mikoba ya Hassan Ali Khaire, ambaye alipigwa kalamu nyekundu mwezi Julai mwaka huu, baada ya kushadidi mvutano wa uongozi baina yake na Rais Farmajo. 

Bunge la Somalia lilipiga kura ya kumtimua Khaire kwa hoja kwamba, ameshindwa kutatua matatizo ya usalama nchini humo, likiwemo suala la kushindwa kuanzisha kikosi cha kitaifa kwa ajili ya usalama wa serikali ya kitaifa na serikali za majimbo. 

Ofisi ya Rais wa Somalia haijatoa maelezo yoyote kuhusu Roble, katika ujumbe wake katika mtandao wa kijamii wa Twitter juu ya uteuzi huo. Khaire na Farmajo wamekuwa wakivutana kwa muda mrefu kuhusu suala la kuakhirishwa au kutoakhirishwa uchaguzi mkuu unaotazamiwa kufanyika mwezi Februari mwaka ujao.

 

Rais Mohamed Abdullahi Mohamed Farmajo wa Somalia

Khaire ambaye aliteuliwa kuwa Waziri Mkuu mwaka 2017, mapema mwezi Julai alisema uchaguzi wa bunge Somalia unapaswa kufanyika mwaka huu kabla ya muhula wa sasa wa bunge kumalizika Disemba. Tume ya Uchaguzi ya Somalia inapendekeza uchaguzi huo ufanyike mwaka ujao kutokana na kuchelewa zoezi la kujitayarisha. Uchaguzi wa rais wa Somalia nao pia umepangwa kufanyika Februari mwakani.

Wakati huohuo, Rais Farmajo na viongozi wa majimbo matano wamemaliza mkutano wa siku tano huko Mogadishu, ambapo wamekubaliana kuhusu marekebisho ya mfumo wa uchaguzi kwa ajili ya uchaguzi wa mwaka 2020/21.

 

 

Tags

Maoni