Sep 18, 2020 10:40 UTC
  • Ethiopia kuwarejesha nyumbani maelfu ya wahajiri kutoka Saudia kwa kuhofia maisha yao

Serikali ya Ethiopia imetangaza kuwa itawarejesha nyumbani wahajiri karibu 2,000 kutoka Saudi Arabia katika wiki zijazo, kutokana na wasiwasi mkubwa wa jamii ya kimataifa juu ya hali mbaya inayoshuhudiwa katika kambi za wahamiaji nchini humo.

Ethiopia inakadiria kuwa makumi ya maelfu ya raia wa nchi hiyo wanaofanyakazi nchini Saudi Arabia wako chini ya mashinikizo makubwa na wengi miongoni mwao wamekwama hapo bila kazi wala kipato.

Hata hivyo Waziri wa Nchi katika Masuala ya Kigeni wa Ethiopia, Tsion Teklu, amesema nchi hiyo haina rasilimali za kuwarudisha nyumbani wahajiri wanaokadiriwa kuwa 14,000 wanaozuiliwa katika kambi za Saudi Arabia ambazo Umoja wa Mataifa umeonya kuwa zina mrundikano mkubwa wa watu na hazina viwango vya afya.

Waziri Teklu amesema Serikali ya Ethiopia ilianza kuwarejesha nyumbni baadhi ya wahajiri hao wiki iliyopita na ina mpango wa kurudisha karibu wengine 2,000, hasa wanawake na watoto, kabla ya katikati ya mwezi ujao wa Oktoba.

Shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch lilisema katika ripoti ya mwezi uliopita kwamba suala la kuwekwa kizuizini wahamiaji ni tatizo la muda mrefu nchini Saudi Arabia.  

Wahajiri wanashikiliwa katika mazingira mabaya nchini Saudia

Mwezi uliopita pia Human Rights Watch iliripoti kuwa makumi ya wahajiri wa Kiethiopia waliokimbia vita kaskazini mwa Yemen wameuawa kwa kupigwa risasi na askari wa mpakani wa Saudi Arabia.
Ripoti ya Human Rights Watch ilisema kuwa maelfu ya wahajiri wa Kiethiopia wanashikiliwa na utawala wa Saudi Arabia katika mazingira mabaya na ya kutisha.

Vilevile Shirika la Wahajiri la Umoja wa Mataifa (IOM) lilisema Jumanne iliyopita kwamba lina wasiwasi kuhusu ripoti kwamba wahamiaji wa Kiethiopia wanashikiliwa katika mazingira yasiyo ya kibinadamu nchini Saudi Arabia.

Tags

Maoni