Sep 18, 2020 10:41 UTC
  • Rusesabagina asema alihadaiwa na kupelekwa Rwanda badala ya Burundi

Paul Rusesabagina anayejulukana kama Shujaa wa filamu ya 'Hotel Rwanda' inayosimulia kisa cha mauaji ya kimbari ya mwaka 1994 nchini Rwanda, anasema kuwa, aliamini alikuwa akisafiri kwenda Burundi kwa mwaliko wa mchungaji wa kanisa, lakini badala yake akahadaiwa na kupelekwa Rwanda na kukamatwa kwa tuhuma za ugaidi.

Rusesabagina alikuwa akizungumza na gazeti la New York Times katika mahojiano ambayo gazeti hilo linasema limeidhinishwa na serikali ya Rwanda na kwsamba yamefanyika mbele ya maafisa wa serikali.

Rusesabagina aliwekwa kizuizini nchini Rwanda mapema mwezi huu na baadaye familia yake ilidai kwamba ametekwa nyara na serikali ya Kigali. Hata hivyo anasema alipanda ndege ya huko Dubai kwa hiari yake mwenyewe akiamini ilikuwa ikielekea Bujumbura, Burundi, ambako alitazamiwa kuzungumza na makanisa kwa mwaliko wa mchungaji wa eneo hilo.

Badala yake, ndege hiyo ilitua katika uwanja wa ndege wa Kigali, ambapo sasa anakabiliwa na mashtaka 13, yakiwemo ya ugaidi, kuhusika katika mauaji na kuunda au kujiunga na kundi la waasi linalotumia silaha dhidi ya nchi ya Rwanda. Vilevile anatuhumiwa kuwa ni mfadhili na kiongozi wa kundi la waasi la MRCD ambalo ni tawi la kijeshi la National Liberation Front (NLF) linalohusisshwa na mashambulizi yaliyoikumba Rwanda mwaka 2018 na 2019. Rwanda ilimkamata msemaji wa NLF, Callixte Nsabimana, mwaka jana.

Paul Rusesabagina 

Wiki iliyopita Serikali ya Rwanda ilisema kuwa Rusesabagina ambaye wakati wa mauaji ya kimbari ya mwaka 1994 alikuwa meneja wa Hoteli ya des Mille Collines mjini Kigali, alitiwa nguvuni kwa kibali cha Polisi ya Kimatifa Interpol.
Paul Rusesabagina alifikishwa mahakamani tarehe 14 mwezi huu wa Septemba chini ya ulinzi mkali wa vyombo vya usalama na kusomewa mashtaka ya ugaidi na kuhujumu usalama wa taifa.

Rusesabagina ambaye amekuwa akiishi uhamishoni tangu 1996, ni mkosoaji mkubwa wa serikali ya Rais Paul Kagame.

Tags

Maoni