Sep 21, 2020 02:27 UTC
  • Covid-19; WHO yaainisha kanuni za kufanyia majaribio dawa za asili za Kiafrika

Huku jitihada za kutafuta chanjo ya ugonjwa wa Covid-19 zikiendelea katika nchi kadhaa duniani, Shirika la Afya Duniani (WHO) limeafiki kanuni za kufanyia majaribio dawa za asili za Kiafrika kwa ajili ya kutibu ugonjwa huo.

WHO imesema kanuni hizo zinalenga kuwasaidia na kuwahamasisha wanasayansi wa Kiafrika kuzifanyia dawa hizo za asili utafiti wa kisayansi, na iwapo itathibiti kuwa ni salama na athirifu, zitaidhinishwa rasmi na shirika hilo kwa ajili ya matumizi. 

Jopo la wataalamu lililoundwa na WHO, Vituo vya Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa wa Afrika (Africa CDC) na Kamisheni ya Masuala ya Kijamii ya Umoja wa Afrika limeafiki protokali za majaribio hayo.

Mwenyekiti wa jopo hilo, Profesa Motlalepula Gilbert Matsabisa amesema utafiti huo umeingia katika marhala ya tatu inayojumuisha uchunguzi wa kubaini usalama wa dawa zenyewe ili kuhakikisha kuwa zinakubalika kote duniani.

Awali WHO iliwatahadharisha watu hususan katika nchi za Afrika dhidi ya kwenda kwa waganga wa kienyeji kutafuta tiba ya corona au kutumia mimea inayodaiwa kutibu ugonjwa huo. 

Miezi michache iliyopita na licha ya kuwepo shaka na upinzani, lakini serikali ya Madagascar iliuza dawa ya asili ya 'Covid Organics' inayodaiwa kutibu maradhi hayo ya kuambukiza. Nchi kadhaa za Afrika zikiwemo Niger, Equatorial Guinea, Senegal, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na Tanzania ziliagiza dawa hiyo kwa ajili ya kuifanyia utafiti. 

Rais Andry Rajoelina wa Madagascar alipozindua 'dawa ya asili ya corona' miezi mitano nyuma

Kadhalika waganga wa kienyeji nchini Tunisia licha ya indhari ya Wizara ya Afya ya nchi hiyo, lakini wameendelea kupata faida kubwa kutokana na mauzo ya mitishamba na dawa za kiasili wanazodai kuwa zinatibu corona.

Walioambukizwa virusi vya corona duniani kote wamepindukia milioni 30, huku walioaga dunia kwa maradhi hayo wakiwa ni zaidi ya laki 9 na 60 elfu. Aidha waliopata afueni baada ya kuambukizwa virusi vya corona duniani ni zaidi ya milioni 21. Idadi ya maambukizi ya ugonjwa wa Covid-19 barani Afrika ni milioni 1.3, ambapo 33, 000 miongoni mwao wameaga dunia.

Tags

Maoni