Sep 21, 2020 08:07 UTC
  • Sudan yatoa sharti la kupatiwa dola bilioni 1 ili ianzishe uhusiano na utawala haramu wa Israel

Duru za habari za Kizayuni zimefichua kuwa, Sudan imeomba kupatiwa msaada wa dola bilioni moja za Kimarekani kama sharti la kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala dhalimu wa Israel.

Mtandao wa habari wa Kiebrania wa Walla umedai kuwa, tayari kumefanyika kikao cha pande tatu baina ya Sudan, Imarati na Marekani ambapo Khartoum imetoa sharti la kupatiwa msaada wa dola bilioni moja za Kimarekani ili ianzishe uhusiano wa kawaida na utawala dhalimu wa Israel.

Ripoti zinaeleza kuwa, endapo Marekani itakubaliana na takwa hilo la Sudan, basi kuna uwezekano katika siku chache zijazo kukatangazwa habari ya kuanzishwa uhusiano wa kawaida baina ya Khartoum na Tel -Aviv.

Haya yanaripotiwa katika hali ambayo, viongozi wa Sudan wamekuwa wakikana tetesi na taarifa zozote zile za kuweko mpango wa nchi hiyo wa kuanzisha uhusiano na utawala ghasibu wa Israel.

Aidha baadhi ya ripoti zinaeleza kuwa, Saudi Arabia na Imarati zimekuwa zikiishinikiza Sudan ili ikubali kuanzisha uhusiano na utawala wa Kizayuuni wa Israel.

Hafla ya kutiwa saini makubaliano ya Bahrain na Imarati ya kuanzisha uhusiano na Israel

 

Nchini Sudan kwenyewe kumekuwa na upinzani mkali wa wananchi na vyama vya upinzani dhidi ya hatua yoyote ile ya nchi hiyo ya kutaka kuanzisha uhusiano na utawala huo ghasibu.

Hivi karibuuni Chama cha Kimomunisti cha Sudan (Sudanese Communist Party) kilitangaza kuwa, kinapinga mpango wowote ule wa kutaka kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala haramu wa Israel.

Chama cha mwanasiasa mkongwe Sadiq al-Mahdi cha The National Umma Party nacho kkimetangaza kupinga hatua yoyote ile ya Khartoum ya kutaka kuanzisha uhusiano wa kawaida na dola hilo bandia.

Maoni