Sep 21, 2020 14:37 UTC
  • Jaji Mkuu wa Kenya amtaka Rais Uhuru Kenyatta kulivunja Bunge

Jaji Mkuu wa Kenya David Maraga Jumatatu ya leo amemshauri Rais Uhuru Kenyatta kulivunja Bunge kwa sababu ya kushindwa kutunga sheria kuhusu usawa wa kijinsia.

Maombi kadhaa yalikuwa yametaka Bunge hilo livunjwe, yakitaja suala la kushindwa majaribio kadhaa ya taasisi hiyo, kutunga Sheria ya Jinsia licha ya maagizo ya korti.

Jaji Mkuu wa Kenya amesema kuwa, ingawa uamuzi huo utasababisha "usumbufu na matatizo ya kiuchumi", lakini ni "dawa mujarabu ya Wakenya wanaotaka kuhamasisha wanasiasa kufuata na kutekeleza kikamilifu mabadiliko ya Katiba."

Jaji Maraga amemwambia Rais Uhuru Kenyatta kwamba: "Wacha tuonje maumivu, ikiwa ni lazima kufanya hivyo, japo tu kwa ajili ya kujikumbusha kama nchi, kwamba machaguo haswa kuhusu utekelezaji wa Katiba, yana gharama zake."

Jaji Mkuu wa Kenya David Maraga

Sheria ya Usawa wa Jinsia ilitolewa katika Katiba ya 2010 na kwa jumla inakusudia kuhakikisha usawa wa kijinsia na usawa katika uteuzi wa nyadhifa mbalimbali serikalini.

Sheria hiyo Ilikuwa moja kati ya mambo  ambayo Bunge lilipaswa kuyafanya ndani ya miaka mitano baada ya kutangazwa mabadiliko ya Katiba, lakini haijatekelezwa hadi sasa, karibu miaka kumi baada ya kupasishwa.

Jaji Mkuu wa Kenya amesema hali hii imeonyesha udhaifu wa msimamo na mwenendo wa Bunge katika suala hilo.

Tags

Maoni