Sep 22, 2020 02:41 UTC
  • Uturuki: Ankara itaendelea kuisaidia serikali ya GNA Libya hata baada ya Sarraj kung'atuka

Uturuki imetangaza kuwa itaendelea kuiunga mkono serikali inayotambuliwa kimataifa ya Libya licha ya Waziri Mkuu Fayez al-Sarraj kutangaza wiki iliyopita kwamba, anapanga kuondoka madarakani mwishoni mwa mwezi ujao.

Msemaji wa Rais Recep Tayyip Erdogan wa Uturuki, Ibrahim Kalin amesema kuwa, misaada ya Uturuki kwa Serikali ya Mwafaka wa Kitaifa ya Libya (GNA) yenye makao makuu Tripoli na makubaliano ya nchi mbili, ambayo ni pamoja na makubaliano ya usalama na makubaliano ya kuweka mipaka baharini yaliyotiwa saini mwaka jana, yataendelea.

Kalin amesema: "Makubaliano haya hayataathiriwa na kipindi hiki cha kisiasa kwa sababu ni maamuzi yaliyofanywa na serikali, sio na mtu binafsi." 

Mwishoni mwa mwaka jana, Ankara ilifikia makubaliano na Serikali ya Mwafaka wa Kitaifa wa Libya (GNA) yanayoipa Uturuki haki ya kutafuta na kuchimba mafuta na gesi katika ukanda wa mashariki mwa Bahari ya Meterania ambako Ugiriki pia inasema sehemu yake kubwa iko chini ya mamlaka ya baharini ya nchi hiyo. 

Ugiriki, Cyprus na nchi nyingine za eneo hilo zimeshutumu makubaliano ya Uturuki na Libya na kuyataja kuwa "haramu". 

Erdogan (kulia) na al Sarraj

Msemaji wa Rais wa Uturuki amesema maafisa wa nchi hiyo watakwenda Tripoli katika siku zijazo kujadili hali ya mambo baada ya tangazo la al-Sarraj.

Al-Sarraj amekuwa akiongoza serikali ya GNA tangu ilipoanzishwa mwishoni mwa mwaka 2015 kutokana na makubaliano ya kisiasa yaliyosimamiwa na Umoja wa Mataifa yenye lengo la kurejesha amani na utulivu Libya baada ya machafuko yaliyofuatia kuangushwa kwa kiongozi wa zamani wa nchi hiyo, Muammar Gaddafi mnamo 2011.

Tags

Maoni