Sep 22, 2020 03:24 UTC
  • Wamisri wamtaka al Sisi ang'atuke madarakani, maandamano yaendelea kwa siku ya pili mfululizo

Wananchi wa Misri jana walifanya maandamano kwa siku ya pili mfululizo wakitaka kukomeshwa utawala wa kijeshi na kuondoka madarakana Rais Abdel Fattah al Sisi wa nchi hiyo.

Maandamano hayo yanafanyika kutokana na wito wa msanii na mfanyabiashara maarufu wa Misri, Muhammad Ali sambamba na hali mbaya ya maisha na kuendelea operesheni ya kubomoa nyumba za raia ambazo serikali ya al Sisi inadai zimejengwa kinyume cha sheria. 

Waandamanaji katika miji mbalimbali ya Misri walikuwa wakipiga nara dhidi ya Rais wa nchi hiyo, Abdel Fattah al Sisi na kuwataka raia wote kujiunga na maandamano hayo.

Wamisri wanamtaka Rais Abdel Fattah al Sisi aondoke madarakani

Makundi na jumuiya mbalimbali za kisiasa zimeapa kwamba zitaendeleza maandamano hayo hadi Misri 'itakapokombolewa' kutoka kwenye mikono ya maghasibu wa utawala ambao wamesema wamelisaliti taifa, kulidhalilisha jeshi na kuitumbukia nchi katika mikataba ya kifisadi.

Tangu aliposhika madaraka ya nchi kupitia mapinduzi ya kijeshi hapo mwaka 2013, Abdel Fattah al Sisi amekuwa akikandamiza harakati zote za wapinzani wa serikali akiungwa mkono au kunyamaziwa kimya na nchi za Magharibi hususan Marekani.

Mashirika na jumuiya za kimataifa zinakosoa sana utawala wa al Sisi kutokana na ukandamizaji mkubwa wa haki za binadamu, uhuru wa kisiasa na kijamii na mbinyo mkubwa unaoshuhudiwa katika maeneo mbalimbali ya nchi hiyo.  

Maoni