Sep 24, 2020 07:52 UTC
  • Rais wa Ghana: Nitafanya jitihada za kuimarisha uhusiano wetu na Iran

Rais Nana Akufo-Addo wa Ghana amesema atafanya juu chini kuimarisha uhusiano wa pande mbili na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Rais wa Ghana amesema hayo leo Alkhamisi katika hafla ya kumuaga Balozi wa Iran mjini Accra, Nosratollah Maleki na kueleza bayana kuwa, "Ghana ina hisia nzuri sana kuhusu Iran."

Rais Nana Akufo-Addo wa Ghana amempongeza mwanadiplomasia huyo wa Iran kwa jitihada zake za kujaribu kuboresha na kufikisha katika kiwango cha juu zaidi uhusiano wa pande mbili wa Tehran na Accra katika kipindi alichohudumu.

Amebainisha kuwa, "Ghana na Iran zinajivunia mambo yenye maslahi ya pamoja na thamani zinazoshabihiana, na zina ushirikiano unaostawi katika nyuga mbalimbali kama afya na elimu."

Kwa upande wake, Balozi wa Iran mjini Accra anayeondoka, Nosratollah Maleki amesema Tehran na Accra zina ushirikiano uliokita mizizi katika nyuga za elimu, siasa na uchumi.

Ameashiria kuhusu safari ya Rais huyo wa Ghana nchini Iran ambayo ilipelekea kusainiwa hati saba za makubaliano ya ushirikiano na kusisitiza kuwa, tayari nchi mbili hizi vikao sita vya kamisheni ya pamoja.

Kuhusu uchaguzi mkuu wa urais unaotazamiwa kufanyika mwaka huu 2020 nchini Ghana, mwanadiplomasia huyo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amelitakia taifa hilo la Kiafrika na serikali mafanikio katika zoezi hilo la kidemokrasia.

 

Tags

Maoni